Sep 23, 2020 08:03 UTC
  • Mapitio ya sababu za kutokea Mapinduzi ya Yemen ya Septemba 21

Sayyid Abdul-Malik Badruddin al-Houthi, Kiongozi wa Ansarullah ya Yemen amesema, Mapinduzi ya Septemba 21 yalikuwa mwanzo wa kuondokana na zama zilizopita za giza na kupiga hatua mbele kuelekea kwenye ujenzi wa mustakabali unaoendana na misingi na thamani za watu wa Yemen.

Katibu Mkuu wa harakati ya Ansarullah ameyasema hayo katika hotuba aliyotoa kwa mnasaba wa maadhimisho ya mwaka wa sita wa Mapinduzi ya Septemba 21.

Sayyid Abdul-Malik Badruddin al-Houthi, Kiongozi wa Ansarullah ya Yemen

Wananchi wa Yemen walianzisha mapambano kwa njia ya maandamano kupinga udikteta wa miaka 33 wa utawala wa Ali Abdullah Saleh. Licha ya uingiliaji wa kila hali wa baadhi ya nchi za Kiarabu na Marekani, mwishowe mapambano ya wananchi wa Yemen yalizaa matunda kwa Abdallah Saleh kuondolewa madarakani. Ijapokuwa kuingia madarakani Abdrabbuh Mansur Hadi halikuwa ndilo takwa la wananchi lakini kulichukuliwa kama ushindi mkubwa kutokana na kuwezesha kung'olewa madarakani Ali Abdullah Saleh. Mansur Hadi alishika hatamu za madaraka Februari 2012; na Septemba 2014, ikiwa ni chini ya muda wa miaka mitatu, naye pia aliachia hatamu za uongozi. Suali muhimu linaloulizwa ni, ilikuwaje na kwa nini Wayemeni walishuhudia mapinduzi mawili ndani ya kipindi cha chini ya miaka mitatu?

Inavyoonyesha, sababu muhimu zaidi ya kushuhudiwa hilo ni kuendelezwa aina ya utawala wa Ali Abdullah Saleh katika kipindi cha uongozi wa Abdurabuh Mansur Hadi. Mansur Hadi alikuwa Makamu wa Abdullah Saleh kwa muda wa miaka 18; na kwa upande mwingine alishika madaraka kwa msaada na uungaji mkono wa Marekani na Saudi Arabia na kwa kupitia mchakato wa uchaguzi wa kimaonesho wa mgombea mmoja. Kwa hivyo baada ya kushika madaraka, hakuwa na uwezo wowote wa kupitisha na kutekeleza maamuzi kwa uhuru; na akamzidi hata Ali Abdullah Saleh katika kutumiwa kuwa mtekelezaji wa sera na maelekezo ya Marekani na Saudia nchini Yemen. Kusema kweli katika kipindi cha utawala wa Abdrabbuh Mansur Hadi Yemen ilikuwa imegeuzwa kuwa eneo la kujifaragua Saudi Arabia na chombo cha kuutumikia utawala wa Aal Saud.

Ali Abdullah Saleh

Wananchi wa Yemen walishuhudia nchi yao ikigeuzwa hivyo ilhali lengo la mapambano yao ya kumng'oa madarakani Ali Abdullah Saleh lilikuwa ni kutaka wawe huru na wajitawale, lengo ambalo lilithibiti kwa Mapinduzi ya Septemba 21 licha ya kuwalazimu kulilinda kwa gharama kubwa zilizotokana na vita vya kivamizi vilivyoanzishwa na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia. Katika hotuba yake kwa mnasaba wa maadhimisho ya mwaka wa sita wa Mapinduzi ya Septemba 21, Katibu Mkuu wa Ansarullah, Sayyid Abdul-Malik Al Houthi alisema: Lengo kubwa zaidi la mapinduzi lilikuwa ni kuwa huru na kujitawala Yemen. Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa Ansarullah mfumo wa kisiasa wa utawala uliokuwepo hapo kabla, haukuweza kuelewa nguvu na uwezo wa wananchi wa Yemen na ukiamini kwamba watu wa nchi hiyo hawawezi kusimama kidete kukabiliana na uingiliaji wa Marekani na kulinda uhuru na kujitawala kwao.

Kuwa tegemezi na kutokuwa huru katika kujiamulia mambo yake Yemen kulikuwa na umuhimu kwa Saudi Arabia, kiasi kwamba baada ya kupita miezi sita tu tangu yalipotokea Mapinduzi ya Septemba 21, nchi hiyo na kwa msaada na uungaji mkono wa moja kwa moja wa Marekani iliishambulia kijeshi Yemen na kuanzisha vita vya kivamizi vinavyoendelea kwa miezi 66 sasa.

Sababu nyingine inayotoa jibu kwa suali la kwa nini Mapinduzi ya Septemba 21 yalitokea nchini Yemen ni kutokuwa na nia ya dhati serikali ya muda ya Mansur Hadi ya kuitisha uchaguzi ili kuundwa serikali ya kudumu. Abdrabbuh Mansur Hadi alichaguliwa kuwa rais wa serikali ya muda Februari 2012 na akashikilia madaraka kwa muda wa miaka miwili. Lakini baada ya kipindi hicho, mnamo Februari 2014 Chama cha Kongresi Kuu ya Watu ya Yemen kilirefusha kipindi cha urais wake kwa mwaka mmoja mwingine, hatua ambayo ilikuwa kinyume cha sheria. Kwa upande mwingine, hata katika kipindi hicho cha mwaka mmoja wa kurefushwa muda wa utawala wa Abdrabbuh Mansur Hadi, serikali yake haikuonyesha ishara wala muelekeo wowote wa kuitisha uchaguzi ili kuundwa serikali ya kudumu. Ni kwa sababu hiyo, katika msimu wa joto wa mwaka 2014 maandamano ya wananchi dhidi ya serikali ya muda ya Mansur Hadi yalianza na kufikia kilele kwa mwafaka uliofikiwa Septemba 21 kati ya serikali ya mpito na Ansarullah ambao ulipelekea harakati hiyo ya wananchi nayo pia kushirikishwa katika mgao wa madaraka ya nchi.

Abdrabbuh Mansur Hadi

Lakini sababu ya tatu iliyopelekea kujiri Mapinduzi ya Septemba 21 ni kwamba serikali ya mpito ya Abdrabbuh Mansur Hadi ilikuwa imeshughulika kufikiria zaidi maslahi ya kisiasa na kimatapo, kiasi cha kutojali na kuzingatia hali za maisha ya watu. Tangu siku Mansur Hadi aliposhika hatamu za madaraka, matatizo ya kiuchumi ya wananchi wa Yemen yalikuwa yakiongezeka siku baada ya siku. Jambo hilo pia lilikuwa cheche iliyochochea moto wa maandamano ya wananchi wa Yemen yaliyolenga kumng'oa madarakani Abdrabbuh Mansur Hadi.../ 

Tags