Sep 25, 2020 02:36 UTC
  • Salman bin Abdulaziz Al Saud
    Salman bin Abdulaziz Al Saud

Mfalme wa Saudi Arabia, Salman bin Abdulaziz Al Saud amekariri madai yake yasiyo msingi dhidi ya Iran katika hotuba yake kwenye kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Katika hotuba hiyo iliyotolewa kwa njia ya video, Mfalme Salman bin Abdulaziz alitoa madai kadhaa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ameituhumu Iran kuwa imeishambulia Saudi Arabia kupitia vita vya Yemen, kuunga mkono ugaidi, kustawisha silaha zinazovuruga amani na usalama wa kikanda na kwamba imekataa suluhu na Saudia. 

Matamshi ya Mfalme Salman katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa yalikuwa na n ujumbe tatu muhimu.

Ujumbe wa kwanza ni kwanza, Saudi Arabia imekasirishwa sana na nguvu kubwa ya Iran na vilevile mabadiliko ya mlingano wa nguvu kwa maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu katika kanda hii ya magharibi mwa Asia. Hasira hizo zinaonekana zaidi katika matamshi ya Mfalme Salman pale alipodai katika hotuba yake kwamba, katika miongo ya karibuni Saudia imenyoosha mkono wa amani kwa Iran na kufanya jitihada za kuwa na uhusiano mwema na Tehran. Salman bin Abdilaziz ametoa madai hayo akijisahaulisha kwamba tangu mwaka 2016 Saudi Arabia ilikata uhusiano wake wa kidiplomasia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ikazishinikiza nchi nyingine kadhaa za Kiarabu zifuate mkondo huo.

Ujumbe wa pili katika hotuba ya Mfalme wa Saudi Arabia katika ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa nii ungaji mkono wake kwa Marekani mbele ya ukosoaji mkubwa wa viongozi na maafisa wa nchi nyingine duniani hususan madola ya Magharibi. Katika hotuba zao kwenye mkutano huo, viongozi wa nchi mbalimbali wamekosoa sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za Marekani katika masuala ya kimataifa na jinsi serikali ya Donald Trump inavyokanyaga sheria za kimataifa na kuzusha mpasuko katika Baraza la Usalama.  

Vibaraka wakitoa mkono wa utiifu (bai'a) kwa Trump

Inaonekana kuwa, Mfalme Salman alipewa jukumu na mabwana zake la kuhakikisha anaelekeza macho ya walimwengu na vyombo vya habari upande wa Iran na kuvizuia kuendelea kukosoa sera na siasa za Marekani.

Ujumbe wa tatu unaopatikana katika hotuba ya Mfalme wa Saudi Arabia ni kwamba Riyadh imeshindwa vita vya Yemen. Saudia ambayo ilianzisha vita hivyo mwezi Machi mwaka 2015 imenasa katika kinamasi cha Yemen na kupatwa na fedheha kubwa kisiasa baada ya kushindwa mbele ya nchi hiyo maskini ya Kiarabu licha ya kuendeleza mashambulizi makali ya miezi 66 sasa dhidi ya taifa hilo ikisaidiwa na madola ya Magharibi kama Marekani na utawala haramu wa Israel. Madai ya Mfalme Salman kwamba mwezi Septemba mwaka jana Iran ilishambulia taasisi za mafuta za Saudia na kwamba inaendelea kuishambulia nchi hiyo kwa kutumia makombora ya balestiki na ndege zisizo na rubani ni kielelezo na ishara ya kushindwa Riyadh katika vita vya Yemen.

Jinamizi la mauaji ya watoto wa Yemen linawaandama watawala wa Saudia

Katika matamshi yake kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Mfalme Salman wa Saudia ametoa wito wa kuzuiwa ustawishaji wa silaha nchini Iran. Hata hivyo hapana shaka kuwa Iran haijaanzisha mashindano ya silaha katika eneo la magharibi wa Asia na wala haikaribishi suala hilo. Jamhuri ya Kiislamu inazalisha silaha kwa kadiri ya mahitaji yake ya kiulinzi, na kinyume chake, utawala wa Aal Saud ambao unashika nafasi ya pili duniani katika safu ya nchi zinazoongoza kwa kununua silaha kwa wingi zaidi, sasa imekuwa ghala kubwa la silaha za nchi za Magharibi hususan Marekani.

Nukta nyingine ya kuashiria hapa katika matamshi ya mfalme wa Saudia katika Baraza Kuu la UN ni madai yake ya kuunga mkono kuundwa nchi huru ya Palestina ilhani Riyadh imeunga mkono na kushajiisha mapatano ya nchi za Imarati na Bahrain na utawala haramu wa Israel unaoikalia kwa mabavu ardhi ya Palestina! Inatupasa pia kueleza kwamba, kama si ruhusa na taa ya kijani ya Saudi Arabia basi nchi ndogo ya Bahrain isingethubutu hata kutaja jina la Israel seuze kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala huo haramu. 

Tags

Maoni