Sep 25, 2020 06:55 UTC
  • Husam Badran
    Husam Badran

Mjumbe wa Idara ya Siasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema kuwa njama ya Muamala wa Karne na uhasama unaofanywa dhidi ya Palestina vimekuwa chachu ya kukurubiana zaidi harakati na makundi ya kupigania ukombozi ya Palestina.

Husam Badran amesisitiza udharura wa kuwepo mapambano ya pande zote ya Wapalestina chini ya uongozi mmoja madhubuti na kusema kuwa mikutano uliowajumuisha pamoja viongozi wa harakati za Fat'h na Hamas nchini Uturuki katika siku za hivi karibuni imekuwa na mafanikio makubwa.

Badran amesema kuwa, harakati za Fat'h na Hamas zimefikia makubaliano kuhusu mustakbali wa Palestina, na kwamba mtazamo wa harakati hizo utatangazwa kwa makundi mengine ya ukombozi wa Palestina hivi karibuni. 

Hamas: Muamala wa Karne umepelekea kuimarika mapambano

Wawakilishi wa harakati za Hamas na Fat'h walikutana Jumanne iliyopita mjini Istanbul huko Uturuki kujadili njia za kuharakisha mapatano na suluhu baina ya makundi yote ya Palestina.

Mwishoni mwa mkutano huo harakati hizo zilitoa taarifa zikisisitiza udharura wa kudumishwa juhudi za kutetea haki za Palestina na kuabiliana na vitisho na changamoto nyingi zilizopo katika njia ya kupata uhuru na kuunda nchi inayojitawala ya Palestina mji wake mkuu ukiwa Quds tukufu.  

Tags

Maoni