Sep 25, 2020 11:17 UTC
  • Algeria: Kadhia ya Palestina ni jambo tukufu; hatuungi mkono kuanzishwa uhusiano na Israel

Msemaji wa serikali ya Algeria amesema kuwa, kadhia ya Palestina ni jambo tukufu na kueleza kwamba, Algiers inaitambua Palestina kuwa miongoni mwa masuala yake muhimu.

Ammar Belhimer ambaye pia ni Waziri wa Mawasiliano wa Algeria amesisitiza kuwa, Algeria inaunga mkono kwa dhati kabisa kadhia ya Palestina.

Kadhalika amesema kuwa, Palestina ni miongoni mwa masuala muhimu ya Algeria na siku zote msimamo wa nchi hiyo kuhusiana na Palestina uko wazi na bayana kabisa.

Msemaji wa serikali ya Algeria amesema kuwa, nchi yake haiungi mkono mkumbo wa baadhi ya mataifa ya Kiarabu ya kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel ambao unatenda jina kila leo dhidi ya Wapalestina.

Ni haki ya Wapalestina kuunda nchi yao huru mji mkuu wake ukiwa Baitul-Muqaddas na hilo sio jambo la kujadiliwa, amesisitiza msemaji wa serikali ya Algeria.

Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria

 

Hivi karibuni pia, Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria akihutubia mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa alisisitiza kuwa, nchi yake iko pamoja na wananchi madhulumu wa Palestina na kwamba itaendelea kusimama nao hadi pale watakapofanikiwa katika malengo yao matukufu.

Aidha siku chache kabla ya hotuba hiyo, Rais huyo wa Algeria alisisitiza kuwa, nchi yake inapinga vikali hatua zozote zile zenye lengo la kuanzisha uhusiano na utawala vamizi wa Israel unaotenda jinai kila leo dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.

Maoni