Sep 27, 2020 07:45 UTC
  • Kushindwa Mustapha Adib kuunda serikali nchini Lebanon; sababu na matokeo yake

Waziri Mkuu wa Lebanon, Mustapha Adib ametangaza kujiuzulu wadhifa wake huo, baada ya kushindwa kuunda serikali na tayari Rais Michel Aoun amekubali kujiuzulu kwake.

Baada ya kujiuzulu Hassan Diab, tarehe 13 mwezi uliopita, Bunge la Lebanon lilipitisha kwa wingi wa kura jina la Mustapha Adib aliyekuwa amependekezwa na Rais Michel Aoun kushika wadhifa wa Waziri Mkuu. Hata hivyo licha ya kupita siku 26 tangu apewe jukumu hilo, Mustapha Adib ameshindwa hata kuwasilisha orodha ya baraza jipya la mawaziri  nchini Lebanon na sasa ametangaza kujiuzulu.

Kushindwa Mustapha Adib kuunda serikali kunajiri katika hali ambayo, shakhsia huyo alikuwa akiungwa mkono ndani na nje ya Lebanon kwa ajili ya kuchukua wadhifa wa Waziri Mkuu. Inaonekana kuwa, kushindwa Mustafa Adib kuunda serikaali kabla ya chochote, jambo hilo linahusiana na ada na mazoea ya kisiasa yanayotawala katika nchi hiyo. Kwa mujibu wa ada na mazoea ambayo yanajulikana kama "sheria ambayo haijaandikwa" nchini Lebanon, ugavi wa madaraka nchini humo unafanyika kwa msingi wa hisa ya makundi na kaumu.

Rais Michel Aoun wa Lebanon

 

Kwa mfano, viti vya Bunge vimegawanywa sawa bin sawia baina ya Waislamu na Wakristo. Aidha viti hivyo vinagawanya sawa kwa sawa baina ya Waislamu wa Kishia na Kisuni. Ugavi na utaratibu huu umekuwa na changamoto mbalimbali nchini Lebanon. Katika uchaguzi wa mwaka 2018, kambi ya muqawama ilipata wingi wa viti vya Bunge baada ya kunyakua viti 68 vya Bunge la nchi hiyo. Hata hivyo serikali iliundwa na mrengo wa al-Mustaqila. Hiyo ni kwa sababu, Waziri Mkuu wa Lebanon anapaswa kuteuliwa kutoka miongoni mwa Waislamu wa Kisuni.

Baada ya kutangazwa Waziri Mkuu mchakato wa kuunda serikali hasa kuhusu wizara muhimu huchukua muda, na baadhi ya mawaziri wakuu kama ilivyokuwa kwa Mustafa Adib hushindwa kuunda baraza la mawaziri. Aidha wengine kama ilivyokuwa kwa Saad al-Harir mwaka 2018, aliweza kuunda serikali baada ya kupita miezi kumi.

Kimsingi ni kuwa, changamoto zinazohusiana na kutaka hisa ya vyeo na uongozi mirengo mbalimbali ya Lebanon hupelekea mchakato wa uundaji serikali kuingizwa matashi ya kisiasa nchini humo. Mustapha Adib pia amesema baada ya kujiondoa katika jukumu la kuunda serikali kwamba: Mimi nilikuwa nikitaka kutotiwa matamshi ya kisiasa suala la kuundwa baraza la mawaziri, ambapo inasikitisha shatrti hili halikufaniwa katika mwenendo wa kuunda serikali mpya.

Hassan Diab alijiuzulu kabla ya Mustapha Adib 

 

Kutaka hisa ya madaraka kumekuwa kukipelekea kutokuwa thabiti makubaliano nchini humo, na hili linahesabiwa kuwa moja ya vigezo vya kisiasa nchini Lebanon.

Sababu nyingine ya kukwama Adib katika kuunda serikali inahusiana na ukwamishaji mambo wa madola ajinabi. Lebanon ni miongoni mwa mataifa ya Kiarabu ambayo uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani unashuhudiwa kwa wigo mpana katika nchi hiyo; na sababu ya hilo ni njama za baadhi ya mataifa ya Kiarabu na Kimagharibi za kutaka kupuuza au kupunguza nafasi muhimu ya kisiasa ya Hizbullah nchini Lebanon. Upinzani huo umekuwa ukifanyika hata baada ya kufanyika uchaguzi kupitia mambo mbalimbali kama kuzuia kuchukuliwa na Hizbullah baadhi ya wizara au kuanzisha na kuchochea maandamano na kuzusha vurugu na machafuko na kuihusisha Hizbullah na changamoto mbalimbali za kiuchumi na kiusalama zinazoikabili nchi hiyo.

Bendera ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon

 

Inaonekana kuwa, hali hii ilimkabili pia Mustapha Adib ambapo baadhi ya madola ya kigeni yaliingilia mchakato wa kuunda baraza la mawaziri kwa lengo la kupunguza nafasi ya Hizbullah.

Nukta nyingine ni kuwa, kushindwa Mustapha Adib kuunda serikali kutakuwa na matokeo hasi. Kipindi cha mpito cha Hassan Diab kitaendelea na hii maana yake ni kuweko serikali dhaifu kwani, serikali hiyo ya mpito haina mamlaka ya kuchukua maamuzi muhimu. Wakati huo huo, wananchi wengi mjini Beirut wameathirika na mlipuko uliotokea mwezi uliopita ambao uliua zaidi ya watu 190 na kujeruhi wengine 6500.

Mkwamo katika kuunda serikali mpya nchini Lebanon, utapelekea kuakhirishwa mipango ya kufuatilia masuala ya wahanga wa mlipuko wa mkubwa wa Beirut. Aidha kufikiwa makubaliano ya kuteuliwa shakhsia mwingine kwa ajili ya kuchukua wadhifa wa waziri Mkuu nchini Lebanon hasa mtu ambaye ataweza kuunda serikali ni jambo ambalo nalo lina vigingi na changamoto zake.

Tags

Maoni