Sep 27, 2020 13:48 UTC
  • Walioshambulia ubalozi wa Marekani mjini Baghdad ni mamluki wa Washington

Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Nujabaa ya Iraq amesema, shambulio lililolenga maeneo jirani na ubalozi wa Marekani mjini Baghdad limefanywa na mamluki wa Marekani yenyewe.

Sheikh Akram al Ka'abi ameeleza katika taarifa kuwa, Muqawama unaelewa fika kwamba kuvilenga vituo vya kidiplomasia ni kosa la wazi kabisa na unaitakidi kuwa kuvilinda vituo hivyo ni jambo lenye ulazima kwa ajili ya kuimarisha uhusiano wa Iraq na nchi mbali mbali ambako kunasaidia ujenzi na ustawi wa nchi.

 Al Ka'abi amesisitiza kuwa, Marekani inawaamuru mamluki wake iliowapa mafunzo na kuwazatit kwa silaha wazishambulie nyumba zilizo jirani na ubalozi wake ili kuchochea fikra za waliowengi na kuchafua jina la Muqawama.

Sheikh Akram Al Ka'abi

Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Nujabaa ya Iraq amesisistizia pia kufungwa vituo vya utoaji mafunzo ya kijeshi vilivyoko kando ya ubalozi wa Marekani mjini Baghdad ambavyo vinatumiwa kuzusha fujo na machafuko na akaeleza kwamba ana matumaini jitihada zinazofanywa kwa nia njema kutaka wanajeshi wavamizi wa Marekani waondoke kikamilifu nchini Iraq zitafanikiwa.

Katika miezi ya karibuni, ubalozi wa Marekani katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad, misafara ya kijeshi na vituo vya askari wa jeshi la kigaidi la nchi hiyo vilivyoko nchini humo vikiwemo vya al Taji na al Balad vimeshambuliwa mara kadhaa.

Wananchi wengi wa Iraq pamoja na makundi na mirengo ya kisiasa na kidini ya nchi hiyo wanataka askari wa jeshi la kigaidi la Marekani waondoke nchini humo; na hata bunge la nchi hiyo limeshapitisha mpango wa kutaka askari hao waondoke katika ardhi ya Iraq.../

Tags

Maoni