Sep 27, 2020 14:03 UTC
  • Afisa wa Fat-h: Nchi za Kiarabu hazitapata manufaa yoyote kwa kufanya mapatano na Israel

Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Harakati ya Fat-h ya Palestina amesema, nchi za Kiarabu hazitapata manufaa yoyote kwa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.

Jibril al Rajoub ameongeza kuwa, baada ya muda kupita nchi za Kiarabu zilizofanya mapatano na utawala wa Kizayuni zitakuja kutambua kuwa zimewatendea jinai Wapalestina.

Al Rajoub amesema, thamani ya muqawama wa wananchi, ambao ni stratejia ya kimapambano ya kukabiliana na utawala wa Kizayuni ina umuhimu mkubwa sana; na akabainisha kwamba mwafaka uliofikiwa karibuni kati ya harakati za Fat-h na Hamas wa kuitisha uchaguzi wa Palestina yote umeonyesha kuwa makundi ya Kipalestina yanapitisha maamuzi yao kwa uhuru.

Jibril al Rajoub

Katika hatua inayopingana kikamilifu na malengo matukufu ya wananchi wa Palestina, tarehe 15 Septemba mawaziri wa mambo ya nje wa Imarati na Bahrain walisaini mkataba wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ikulu ya White House, mjini Washington mbele ya rais wa Marekani Donald Trump.

Hatua hiyo ya Abu Dhabi na Manama ya kuutambua utawala haramu wa Israel na kuanzisha nao uhusiano rasmi wa kidiplomasia imelaaniwa na kukosolewa vikali katika Ulimwengu wa Kiislamu.../

Tags

Maoni