Sep 29, 2020 03:27 UTC
  • Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu atakiwa ajiuzulu

Katibu Mkuu wa Kamati ya Utendaji ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO amelaani vikali matamshi aliyotoa hivi karibuni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Ahmad Abul Ghaith kuhusu kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.

Mbali na kulaani matamshi hayo ya Abul Ghaith, Saeb Erekat amesisitizia pia ulazima wa Katibu Mkuu huyo wa Arab League kujiuzulu mara moja.

Erikat amebainisha kuwa, Ahmad Abul Ghaith amepoteza itibari aliyokuwa nayo na kwa hivyo hawezi kuendelea kuwa Katibu Mkuu wa Arab League.

Siku ya Jumapili, Katibu Mkuu huyo wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu alitoa kauli ya kukaribisha makubaliano ya kuaibisha yaliyofikiwa kati ya nchi mbili za Kiarabu za Imarati na Bahrain na utawala ghasibu wa Kizayuni wa Israel na kudai kwamba, makubaliano hayo yamesitisha mpango wa utawala huo haramu wa kuvamia na kukalia kwa mabavu baadhi ya maeneo ya Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan.

Saeb Erekat

Katika hatua inayopingana kikamilifu na malengo matukufu ya wananchi wa Palestina, tarehe 15 Septemba mawaziri wa mambo ya nje wa Imarati na Bahrain walisaini mkataba wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ikulu ya White House, mjini Washington mbele ya rais wa Marekani Donald Trump.

Hatua hiyo ya Abu Dhabi na Manama ya kuutambua utawala haramu wa Israel na kuanzisha nao uhusiano rasmi wa kidiplomasia imelaaniwa na kukosolewa vikali katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imesema, makubaliano hayo ni "hatari" na sawa na "zawadi ya bure" ambayo Imarati na Bahrain zimeutunukia utawala bandia wa Israel kwa sababu ya jinai unazowatendea Wapalestina.

Tawala za Kiarabu zinachaharika kuanzisha uhusiano wa Kiarabu na Israel wakati kwa miaka na miaka sasa, mbali na utawala huo wa Kizayuni kuwakandamiza wananchi madhulumu wa Palestina, umevamia na kukalia kwa mabavu pia maeneo mengi ya ardhi za Waarabu na Waislamu.../

Maoni