Sep 30, 2020 04:39 UTC
  • Amir wa Kuwait, Sheikh Sabah (91) aaga dunia nchini Marekani

Amir wa Kuwait, Sheikh Sabah al-Ahmad al-Jaber al-Sabah ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 91.

Al-Sabah aliaga dunia jana Jumanne akiwa katika hospitali moja nchini Marekani alikoenda kutibiwa. 

Akithibitisha habari hizo, Sheikh Ali Jarrah al-Sabah, Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo ya Kiarabu amesema, "kwa masikitiko makubwa na huzuni, tunatangaza kifo cha Sheikh Sabah al-Ahmad al-Jaber al-Sabah, Amir wa Kuwait."

Sheikh al-Sabah ambaye alifahamika zaidi kama msanifu wa sera za nje za enzi hizi nchini Kuwait na pia msuluhishi na mpenda amani, alizaliwa mwaka 1929.

Alitawazwa kuwa Amir wa Kuwait Januari mwaka 2006, baada ya kifo cha mtangulizi wake Sheikh Jaber al-Sabah. Alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Kuwait kuanzia mwaka 1963 hadi 2003, na kisha akateuliwa kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo.

Amir wa Kuwait aliyeaga dunia, Sheikh Sabah al-Ahmad al-Jaber al-Sabah 

Agosti mwaka jana 2019, serikali ya Kuwait ilitangaza kuwa Sheikh al-Sabah anaugua ugonjwa ambao haukutajwa, na kwamba alilazimika kulazwa hospitalini.

Julai mwaka huu 2020, Amir huyo wa Kuwait alipelekwa mjini Rochester, katika jimbo la Minnesota nchini Marekani kwa ajili ajili ya matibabu baada ya kufanyiwa upasuaji.

 

Tags