Sep 30, 2020 08:04 UTC
  • Iran yatuma salamu za rambi rambi baada ya kuaga dunia Amir wa Kuwait

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametuma salamu za rambi rambi kufuatia kuaga dunia Sheikh Swabah al-Ahmad Jabir as-Swabah, Amir wa Kuwait.

Katika ujumbe kupitia Twitter, Zarif amesema: "Tumeumia moyo kufuatia kuaga dunia Sheikh Swabah al-Ahmad Jabir as-Swabah, Amir wa Kuwait, ambaye alikuwa akiwakilisha taswira ya misimamo ya wastani ya Kuwait na eneo. Tunamuomba Mwenyezi Mungu amrehemu na tunaitakia serikali na watu wa Kuwait usalama, uthabiti na ustawi chini ya serikali mpya."

Wakati huo huo, mashauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametuma salamu za rambi rambi kwa serikali na watu wa Kuwait kufuatia kuaga dunia Sheikh Swabah al-Ahmad Jabir as-Swabah.

Ali Larijani, mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amemtumia ujumbe Amir mpya wa Kuwait  Sheikh Nawaf al-Ahmad al-Jaber al-Swabah na kusema marehemu Sheikh Swabah al-Ahmad Jabir as-Swabah alikuwa akisisitiza sana kuhusu uhusiano wa kidugu baina ya Iran na Kuwait.

Amir mpya wa Kuwait Sheikh Nawaf al-Ahmad al-Jaber al-Sabah 

Aidha amemtaja kiongozi huyo aliyeaga dunia wa Kuwait kuwa aliyekuwa na nafasi chanya katika utatuzi wa matatizo ya kieneo. Larijani pia amemtakia mafanikio Amir mpya wa Kuwait.

Sheikh Swabah al-Ahmad Jabir as-Swabah, Amir wa Kuwait  aliaga dunia hapo jana Jumanne tarehe 29 Septemba.

Sheikh Swabah al-Ahmad Jabir as-Swabah ametawala Kuwait kwa miaka 14 yaani tangu mwaka 2006 hadi wakati wa kuaga kwake.

 

Tags