Oct 05, 2020 02:33 UTC
  • Sababu za kujiuzulu Waziri Mkuu wa Jordan

Mfalme Abdullah wa Pili wa Jordan amekubali kujiuzulu kwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Omar al-Razzaz na kumuamuru kukaimu nafasi hiyo hadi litakapoundwa baraza jipya la mawaziri.

Omar al-Razzaz aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Jordan Agosti mwaka 2018 baada ya kufutwa kazi mtangulizi wake, Hani Mulki. Kujiuzulu au kufanyiwa marekebisho serikali ya Jordan si jambo jipya wala geni. Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita serikali ya Jordan ilifanyiwa marekebisho makubwa mara mbili, na ya mwisho ilikuwa Oktoba mwaka jana. Kabla ya hapo pia Hani Mulki aliyekalia kiti cha Waziri Mkuu kwa karibu miezi 20 alilifanyia marekebisho mara tatu baraza lake la mawaziri na mwishowe akalazimika kung'atuka madarakani yeye mwenyewe. 

Kuna sababu zinazofanana za kujiuzulu mara kwa mara mawaziri wakuu na mawaziri wa serikali ya Jordan. Sababu kuu na ya msingi ni kuwa, nchini Jordan madaraka yote ya nchi yako mikononi mwa mfalme, lakini Waziri Mkuu na baraza lake la mawaziri ndilo lenye jukumu la utendaji. Kimsingi Waziri Mkuu nchini humo hana uhuru wala mamlaka ya kuchukua maamuzi bila ya idhini ya mfalme, lakini pale mambo yanapokwenda mrama na kukabiliwa na malalamiko ya wananchi, waziri mkuu na serikali ndio wanaolaumiwa na kuwa wahanga. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana umri wa serikali za Jordan huwa mfupi kama ilivyoshuhudiwa kwa serikali za Omar al-Razzaz na Hani Mulki ambazo kwa pamoja zimekuwa madarakani kwa kipindi cha chini ya miaka minne. 

Wajordan wakipinga sheria mpya ya ushuru

Sababu nyingine ya kujiuzulu serikali za Jordan ni changamoto nyingi za kiuchumi na malalamiko mengi ya wananchi. Sababu hii imekuwa na nafasi kubwa sana hususan kuhusu serikali ya Omar al-Razzaz ambayo tangu miezi kadhaa iliyopita imekuwa ikiandamwa na maandamano ya wananchi wanaolalamikia hali mbaya ya kiuchumi. Wajordan walianza kufanya maandamano wakilalamikia ongezeko la bei ya nishati na utekelezaji wa sheria mpya ya ushuru, lakini maandamano hayo yalisitishwa kutokana na sheria kali za kupambana na maambukizi ya virusi vya corona. Hata hivyo kushadidi matatizo ya kiuchumi kelichochea tena maandamano ya Wajordan ambayo mara hii yaliongozwa na tabaka la walimu. Vilevile zaidi ya wanasiasa 500 mashuhuri wa Jordan wakiwemo mawaziri wawili wakuu wa zamani wa nchi hiyo, Abdulsalam Al-Majali na Taher Nashat al-Masri, wamesaini waraka uliotumwa kwa mfalme Abdullah wa Pili wa nchi hiyo wakilalamikia hali mbaya ya kisiasa na kiuchumi. Waraka huo ulisisitiza kuwa, sera za serikali ya al-Razzaz zimetatiza zaidi hali ya kiuchumi na kimaisha ya taifa la Jordan.

Sababu ya tatu ya kujiuzulu sererikali za Jordan ni kuvunjwa Bunge la nchi hiyo. Tarehe 25 Septemba Mfalme Abdullah wa Pili wa Jordan alilivunja bunge la nchi hiyo, na kwa mujibu wa katiba, serikali ya Amman pia ilipaswa kuvunjwa wiki moja baadaye. Mfalme Abdullah amesema sababu ya uamuzi huo ni kutayarisha mazingira ya kuitishwa uchaguzi Bunge. Tume ya Uchaguzi ya Jordan imetangaza kuwa, uchaguzi huo utafanyika tarehe 10 Novemba mwaka huu wa 2020. Uchaguzi wa Bunge la Jordan hufanyika mara moja kila baada ya miaka minne.

Askari usalama wa Jordan wakikabiliana na waandamanaji

Nukta ya mwisho ya kuashiria hapa ni kwamba kwa mujibu wa katiba ya Jordan, Bunge la taifa linapovunjwa, serikali pia huvunjwa katika kipindi kisichozidi wiki moja, na waziri mkuu wa kipindi hicho hawezi tena kuunda serikali ijayo. Kwa msingi huo Omar al-Razzaz hataweza kuunda serikali mpya; hivyo ataendelea kukaimu nafsi hiyo hadi waziri mkuu mpya atakapoteuliwa.       

Tags