Oct 12, 2020 03:07 UTC
  • Ripoti: Wanawake na watoto zaidi ya elfu 13 wa Yemen ni wahanga wa mashambulizi ya Saudia

Taasisi moja ya kutetea haki za binadamu nchini Yemen imetangaza kuwa wanawake na watoto zaidi ya elfu 13 wa Kiyemeni wameuawa katika mashambulizi ya muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia nchini humo.

Taasisi ya Haki za Binadamu ya Insaf ambayo inatetea haki za watoto na wanawake wa Yemen jana ilitoa ripoti na kueleza kuwa, idadi sahihi ya wanawake na watoto wa Yemen waliouliwa na kujeruhiwa hadi kufikia Ijumaa ya tarehe 9 Oktoba mwaka huu ni elfu 13 na 73.  

Taasisi hiyo ya haki za binadamu imeeleza kuwa, wanawake 5,183 na watoto 7,891 wa Yemen wameuawa na kujeruhiwa katika mashambulizi ya Saudi Arabia na washirika wake tangu muungano huo uanzishe hujuma zake katika nchi hiyo maskini ya Kiarabu.  

Wanawake na watoto; wahanga wakuu wa mashambulizi ya muungano vamizi wa Saudia huko Yemen  

Ripoti ya taasisi ya haki za binadamu ya Insaf imeongeza kuwa, mamia ya vituo vya afya vya wanawake na watoto pia vinakaribia kufungwa baada ya muungano vamizi wa Saudia kuzuia kuingizwa nishati nchini Yemen na kwamba suala hilo litasababisha maafa makubwa ya kibinadamu. 

Katika ripoti hiyo, taasisi ya haki za binadamu ya Insaf imeeleza kuwa, mashambulizi ya Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya taasisi  za elimu za Yemen pia yamewaathiri karibu wanafunzi milioni mbili. Taasisi  hiyo imetaka kufanyike uchunguzi usioegemea upande wowote kuhusu jinai zilizofanywa na muungano vamizi wa Saudia na kuhukumiwa wahusika wa jinai hizo. 

Tags