Oct 15, 2020 08:08 UTC
  • Imarati yasema Wapalestina hawana shukrani kwa kukosoa uhusiano na Israel

Afisa mmoja wa ngazi za juu wa Umoja wa Falme za Kiarabu amewashutumu vikali wananchi wa Palestina na kudai kuwa hawana shukrani wala hawatambui fadhila, kutokana na hatua yao ya kupinga hatua ya Imarati ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Anwar Gargash, Waziri wa Mambo ya Nje wa Imarati amesema hayo baada ya Balozi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina mjini Paris, Salman El Herfi kulaani hatua ya mataifa mawili ya Kiarabu ya Imarati na Bahrain ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Gargash amesema, "sikushangazwa na matamshi ya Balozi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina nchini Ufaransa kwa kuwa hana utiifu, muamana wala shukrani kwa Imarati."

Balozi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina mjini Paris, Salman El Herfi  hivi karibuni aliliambia jarida la Ufaransa la Le Point kuwa, Imarati na Bahrain zimegeuka na kuwa Waisraeli hata kuwashinda Waisraeli wenyewe kwa hatua yao ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Tel Aviv.

Hafla ya utilianaji saini tawala za Imarati na Bahrain kwa ajili ya kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel

Baada ya Imarati na Bahrain kutangaza uamuzi wa kiuhaini na usaliti wa kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni, tarehe 15 Septemba, nchi hizo mbili ndogo za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi zilisaini rasmi mikataba ya kuanzisha uhusiano huo wa kidiplomasia na kuutambua rasmi utawala bandia wa Israel katika hafla iliyofanyika Ikulu ya White House na kuhudhuriwa na Rais wa Marekani Donald Trump na Waziri Mkuu wa utawala huo wa Kizayuni Benjamin Netanyahu.

Ulimwengu wa Kiislamu bali hata baadhi ya nchi zisizo za Waislamu kama Afrika Kusini zimeendelea kulaani kitendo hicho cha kisaliti cha Bahrain na Imarati.

Tags