Oct 18, 2020 06:41 UTC
  • Uungaji mkono wa kisiasa wa watu wa Iraq kwa Harakati ya Hashdu sh-Sha'abi

Hatua ya mwanachama mmoja wa chama cha Demokrasia cha Kusdistan KDP ya kuivunjia heshima Harakati ya Kujitolea ya Wananchi wa Iraq, Hashdu sh-Sha'abi, imekabiliwa na radiamali kali ya kisiasa ya wananchi hao ambao wameandamana na hata kuchoma moto ofisi ya chama hicho mjini Baghdad.

Hoshyar Zebari, waziri wa zamani wa fedha wa Iraq na ambaye pia ni mwanachama wa ngazi ya juu katika chama cha KDP, mbali na kulituhumu kundi la Hashdu sh-Sha'abi kuwa lilihusika na mashambulio ya karibuni ya maroketi dhidi ya vituo vya Marekani nchini Iraq, ametoa pia matamshi ya dhararu na udhalilishaji dhidi ya kundi hilo kwa kulifananisha na kundi la kigaidi la Daesh.

 Daesh ilivamia na kuuteka mji wa Mosul makao makuu ya mkoa wa Ninawa (Nineveh) mnamo mwaka 2014, uvamizi ambao ulitoa pigo jipya la kijeshi, kijamii na kisiasa kwa watu wa Iraq. Kufuatia uvamizi huo wa kigaidi, Ayatullah Sistani, marja' mkuu wa Iraq alitoa fatwa ya kubuniwa harakati ya wananchi ambayo ilipewa jina la Hashdu sh-Sha'abi.

Baada ya kubuniwa kundi hilo la wananchi, taratibu harakati ya mapambano ilianza dhidi ya ugaidi wa Daesh ambapo baada ya kupita miaka minne tokea libuniwe, lilifanikiwa kuendesha mapambano makali dhidi ya magadi wa Daesh na hatimaye kuwashinda na hivyo kukomboa ardhi yote iliyokuwa imetekwa na kuvamiwa na magaidi hao wanaoungwa mkono na nchi za Kiarabu na za Magharibi na hasa Marekani. Hakuna mtu yoyote aliye na shaka kwamba Hashdu sh-Sha'abi ilitoa mchango mkubwa katika kuwashinda magaidi wa Daesh ambapo ilipoteza maisha ya wafuasi wake wengi katika mapambano hayo.

Hoshyar Zebari

 

Pamoja na hayo lakini vibaraka wa nchi za Magharibi na wafuasi wa makundi ya kikabila na kimedhehebu huko Iraq daima wamekuwa wakifanya uchochezi na kueneza fitina dhidi ya harakati hiyo ya mapambano ya Kiislamu. Kuvunjiwa heshima harakati hiyo kabla ya jambo jingine lolote, kunatokana na msimamo wake ulio huru kuhusu masuala muhimu ya Iraq na sisitizo lake la kulindwa uhuru wa kisiasa na kiusalama wa nchi hiyo. Msimamo huo bila shaka unawakera baadhi ya watu ndani ya Iraq ambao wanafuata na kushajiisha uingiliaji wa nchi za Magharibi na Kiarabu zikiongozwa na Saudi Arabia katika masuala ya ndani ya Iraq.

Hii si mara ya kwanza kwa Hashdu sh-Sha'abi kutuhumiwa na kuvunjiwa heshima kwa namna hiyo nchini Iraq. Mara tu baada ya kushindwa kijeshi magaidi wa Daesh, Marekani na Saudi Arabia pamoja na vibaraka wao waliituhumu Hashdu sh-Sha'abi kuwa ilihusika na baadhi ya kashfa za kimaadili na kiuchumi katika maeneo ya Wasuni, bila kutoa dalili yoyote ya maana.

Kabla ya kufanyika uchaguzi wa bunge pia wapinzani wa Hashdu sh-Sha'abi walifanya juhudi kubwa za kueneza uvumi na uzushi dhidi ya Hashdu sh-Sha'abi ili kuizuia isishiriki katika uchaguzi huo lakini muungano wa al-Fat'h ambao uliungwa mkono na harakati huyo ulipata ushindi mkubwa katika uchaguzi huo baada ya muungano wa Sairoun kuchukua nafasi ya kwanza.

Duru mpya ya tuhuma dhidi ya Hashdu sh-Sha'abi imeanza katika hali ambayo kwa upande mmoja Marekani na askari wake wako chini ya mashinikizo makubwa kufuatia matakwa ya Wairaki wanaoshinikiza waondoke nchini humo mara moja, na kwa upande wa pili maeneo ya kidiplomasia yamekuwa yakishambuliwa na baadhi ya makundi ya Iraq, ambapo Hashdu sh-Sha'abi pia imeyalaani.

Hashdu sh-Sha'abi wakiwa katika medani ya vita dhidi ya magaidi wa Daesh

Tuhuma na matusi haya mapya ya Hoshyar Zebari, ambaye alihudumu katika serikali ya Haidar al-Abadi kama waziri wa fedha, yamekabiliwa na radiamali kali ya kisiasa ya Wairaki. Wanasiasa wengi wa nchi hiyo wamelaani matamshi hayo ya dharau na kejeli na kumkumbusha Zebari nafasi muhimu ya harakati hiyo ya kiislamu na kitaifa, katika kulinda usalama wa nchi hiyo, yakiwemo maeneo ya Wakurdi.

Katika uwanja huo, Jassim al-Ulyawi, mmoja wa viongozi wa ngazi za juu katika Muungano wa an-Nasr unaofungamana na  Haidar al-Abadi, Waziri Mkuu wa zamani wa Iraq, ameisifu sana harakati ya Hashdu sh-Sha'abi kutokana na mchango wake katika kulinda usalama wa Wairaki dhidi ya ugaidi wa Daesh na kuandika kwamba: Maadui wa Iraq hawataki kuona nchini humo kundi lenye nguvu kama hilo ambalo liko tayari wakati wowote kujitolea kwa ajili ya kupambana na migogoro ya kiusalama, kwa sababu lengo lao kuu ni kuifanya Iraq iendelee kuwa dhaifu mbele ya adui.

Tags