Oct 19, 2020 15:35 UTC
  • Mohammad Shtayyeh
    Mohammad Shtayyeh

Waziri Mkuu wa Palestina amesema kuwa kitendo cha kuruhusiwa ujumbe wa Imarati kuingia ndani ya Msikiti wa al Aqsa huku Wapalestina wakizuiwa kuswali katika msikiti huo, kinauma sana.

Mohammad Shtayyeh amesema kuwa, inasikitisha kuona ujumbe wa baadhi ya nchi za Kiarabu ukiruhusiwa kuingia katika Msikiti wa Aqsa wakati utawala haramu wa Israel ukiwazuia Wapalestina kutekeleza ibada ya Swala katika eneo hilo takatifu.

Waziri Mkuu wa Palestina ameongeza kuwa, kuingia katika eneo hilo takatifu kunapaswa kufanyika kupitia mlango wa Wapalestina ambao ndio wamiliki halisi wa Msikiti wa al Aqsa.

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa Jumapili ya jana Wapalestina wanaoishi Quds Tukufu waliutimua ujumbe wa Imarati uliongia katika Msikiti wa al Aqsa chini ya ulinzi wa polisi wa utawala haramu wa Israel.

Ripoti zinasema, Wapalestina waliokuwa na hasira waliwafukuza Waimarati hao wakati walipokuwa wakitembelea eneo Qubbatu Sakhrah na kupiga picha ndani ya msikiti huo mtakatifu na kuwataka waondoke eneo hilo mara moja.

Wapalestina hao walikuwa wakipiga nara zinazopinga hatua ya Imarati ya kuanzisha uhusiano rasmi na utawala haramu wa Israel. 

Tarehe 15 Septemba mwaka huu, Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Bahrain walitia saini makubaliano ya kutangaza uhusiano wa kawaida baina ya nchi zao na utawala ghasibu wa Israel.

Tags

Maoni