Oct 20, 2020 08:21 UTC
  • Umuhimu na malengo ya mabadiliko yaliyofanywa na Mfalme Salman katika Kamati ya Maulamaa na Baraza la Ushauri

Mfalme Salman bin Abdul Aziz wa Saudi Arabia ametoa dikrii kadhaa akibadilisha wajumbe wa Kamati ya Maulama Wakubwa, Baraza la Ushauri na maafisa kadhaa wa mahakama za nchi hiyo.

Mabadiliko hayo yaliyofanywa na Mfalme Salman yanaweza kuchungumzwa kwa kutilia maanani nafasi ya taasisi hizo na malengo ya mabadiliko yenyewe.

Katika mtazamo wa umuhimu na nafasi ya taasisi hizo inatupasa kusema kuwa, Kamati ya Maulama Wakubwa na Baraza la Ushauri ni miongoni mwa asasi ambazo hazina nguvu nchini Saudi Arabia na zaidi ni taasisi za kutoa ushauri. Hata hivyo maamuzi ya Kamati ya Maulama Wakubwa yana umuhimu kwa watawala wa Saudia. Wajumbe wote 21 wa kamati hiyo huteuliwa na mfalme, na asasi hiyo ndiyo chombo cha juu zaidi cha kidini nchini Saudi Arabia, na kazi yake kuu ni kutoa fatwa.

Mfalme wa zamani wa Saudi Arabia Abdullah bin Abdul Aziz alifanya mabadiliko katika asasi hiyo. Kabla ya Mfalme Abdullah kushika madaraka ya nchi, wajumbe wote wa Kamati ya Maulama Wakubwa ya Saudia walikuwa wanazuoni wa madhehebu ya Hanbali, hivyo, mabadiliko hayo yaliwajumuisha maulama wa madhehebu za Shafi, Maliki na Hanafi katika kamati hiyo. Kwa sasa baraza hilo la maulama linaongozwa na Abdul Aziz Aal al Sheikh. 

Maulama wa Saudia

Mabadiliko makubwa yaliyofanyika katika kazi za Kamati ya Waulama Wakubwa tangu Mfalme Salman aliposhika madaraka na kumfanya mwanaye, Muhammad bin Salman, kuwa mrithi wake, ni "kuiserikalisha" zaidi kamati hiyo. Mtaalamu wa masuala ya Saudi Arabia, Kamran Karami, anasema: "Mwishoni mwa mwaka 2016 Mfalme Salman alifanya mabadiliko katika Kamati ya Maulama, akawaondoa baadhi ya wanazuoni wahafidhina katika kamati hiyo na kuwaingiza wale wenye misimamo ya "kisasa"; matokeo yake ni kulifanya baraza hilo kwenda sambamba na maamuzi ya Mfalme Salman na mwanaye, Bin Salman."

Kwa hakika Baraza la Maulama Wakubwa la Saudia lilikuwa chombo cha taasisi ya kisiasa ya nchi hiyo kinachohudumia serikali ya Riyadh, lakini katika miaka 5 ya karibuni nafasi ya chombo hicho imekuwa ya kimaonyesho zaidi.

Vilevile Muhammad bin Salman amefanya mabadiliko katika masuala ya kidini na kijamii nchini Saudi Arabia ambayo katika hatua ya kwanza ilibidi yapasishwe na hata kutolewa fatwa na Kamati ya Maulama Wakubwa ya nchi hiyo. Hata hivyo mrithi huyo wa ufalme alilipuuza baraza hilo la wanazuoni na kivitendo analitumia kwa ajili ya kuhudumia maslahi na malengo yake.

Baraza la Ushauri la Saudia pia ni miongoni mwa asasi ambazo wajumbe wake wote 150 huteuliwa na mfalme wa nchi hiyo, na kazi yake kuu ni kutoa ushauri kwa mfalme ambaye ahalazimiki kufuata au kutekeleza ushauri huo.

Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Maulama Saudia

Kuhusu malengo ya mabadiliko yaliyofanywa katika taasisi hizo inatupasa kusema kuwa, yamefanyika kwa shabaha ya kuwasimika watu wanaoaminiwa na Mfalme Salman kwa shabaha ya kumkalisha kwenye kiti cha ufalme mwanaye, Muhammad bin Salman. Katika mwaka mmoja uliopita Mfalme Salman bin Abdul Aziz amefanya mabadiliko mengi katika asasi za Saudi Arabia na kubadilisha viongozi na watendaji wake; mfano wa suala hilo ni pamoja na kubadilishwa kamanda wa majeshi ya Saudia na idadi kubwa ya maafisa wa juu wa Wizara ya Ulinzi. Hivyo; mabadiliko yaliyofanyika katika Kamati ya Maulama Wakubwa, Baraza la Ushauri na mahakama za la Saudi Arabiani katika mlolongo mabadiliko yanayoendelea katika kipindi cha mwaka mzima uliopita nchini Saudi Arabia.  

Maoni