Oct 21, 2020 06:18 UTC
  • Indhari ya UN kuhusu hali mbaya ya Yemen na kuendelea jinai za Muungano wa Saudia kwa uungaji mkono wa Magharibi

Mnamo mwezi Machi 2015, Saudi Arabia ikishirikiana na Imarati ilianzisha vita vya kidhalimu dhidi ya wananchi wa Yemen kupitia muungano wao wa pamoja wa kijeshi; na hadi sasa muungano huo vamizi umeshaua na kujeruhi makumi ya maelfu ya watu nchini humo.

Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya nazo pia zina mchango katika vita hivyo kutokana na misaada ya kilojistiki, kiintelijensia na kijeshi zinayotoa kwa Saudia na Imarati.

Katika hali hiyo, Umoja wa Mataifa umelazimika kutoa indhari kutokana na hali ya Yemen kuzidi kuwa mbaya. Siku ya Jumatatu, umoja huo ulitangaza kuwa, ikiwa hautapatiwa mchango zaidi wa fedha, ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, utalazimika kupunguza shughuli zake kuu unazoendesha nchini Yemen.

Stéphane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema , "uhaba wa bajeti umelemaza operesheni za misaada ya kibinadamu nchini Yemen. Hivi sasa shughuli 16 muhimu kati ya 41 zinazoendeshwa na Umoja wa Mataifa zimepungua au kusitishwa kikamilifu; na ikiwa haitapatikana bajeti ya ziada, ifikapo mwishoni mwa mwaka, shughuli zingine 26 zitasitishwa au zitapunguza huduma zinazotoa." Dujarric amebainisha kuwa, "hadi sasa ni asilimia 42 tu ya bajeti ya mpango wa kukidhi mahitaji ya kibinadamu nchini Yemen imepatikana, ambacho kitakuwa ni kiwango cha chini kabisa ifikapo mwishoni mwa mwaka."

Stéphane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa UN

Ijapokuwa Umoja wa Mataifa umefanya juhudi ili kufanikisha usitishaji mapigano katika vita angamizi vya Yemen na kuanzisha mazungumzo ya kisiasa ili pande mbili zinazopigana ziweze kufikia mapatano na kupunguza machungu na mateso wanayopata raia wa nchi hiyo iliyoathiriwa na vita, lakini nchi zinazounda muungano vamizi wa kijeshi wa Saudia zimekiuka usitishaji vita na kupuuza mara kadhaa makubaliano yaliyofikiwa na pande hizo. Tajiriba ya huko nyuma imeonyesha kuwa, muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia pamoja na vikosi vya Abdrabbuh Mansur Hadi vinavyoungwa mkono na utawala wa Aal Saud vimekuwa havijali mipango inayopendekezwa na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kusitisha vita; na badala yake vinaendelea kukoleza moto wa vita nchini Yemen.

Wakati hayo yanajiri, ni wazi kwamba muungano vamizi wa Saudia usingeweza kuendeleza vita angamizi dhidi ya Yemen bila misaada na uungaji mkono wa siri na wa dhahiri wa nchi za Magharibi. Shirika la Msamaha Duniani, Amnesty International limeshauri katika ripoti yake kwamba, badala ya nchi za Magharibi kufikiria faida nono zinayopata kutokana na uuzaji silaha, zijali zaidi na kuyapa kipaumbele maisha ya mamilioni ya raia wa Yemen pamoja na wajibu wa kisheria zilionao nchi hizo. Ukweli wa mambo ni kuwa, kama si hatua zinazochukuliwa na Marekani na nchi kadhaa za Ulaya ikiwemo Ufaransa, Uingereza, Ujerumani, Italia n.k za kutuma shehena kwa shehena za silaha na zana za kijeshi huko Yemen, muungano vamizi wa kijeshi wa Saudia na Imarati usingeweza kuendeleza vita vya kidhalimu dhidi ya wananchi madhulumu wa Yemen, ambavyo kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa vimesababisha moja ya maafa makubwa zaidi ya kibinadamu katika karne ya 21. Ni kama alivyosema mtaalamu wa masuala ya kisiasa Barbara Valey kwamba: Marekani na Uingereza ndio wanaobeba dhima ya vita vyenye maafa makubwa na jinai za kivita nchini Yemen.

Malalamiko ya Amnesty Internation kwa hatua ya UK kuendelea kuuzia silaha muungano wa kijeshi wa Saudia

Lakini pamoja na hayo, nchi hizo hizo za Magharibi zinafanya kila njia kuhepa kuchangia bajeti ya fedha, inayohitajika kwa ajili ya mipango ya utumaji misaada ya Umoja wa Mataifa nchini Yemen kupitia operesheni za huduma za kibinadamu. Indhari mpya ya msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nayo pia imetolewa katika muelekeo huo.

Hii ni pamoja na kwamba, madola ya Magharibi zikiwemo nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na Marekani zimesikika mara kadhaa zikidai kuwa, zinataka kusitishwa vita na mapigano nchini Yemen. Hata hivyo ukweli wa kauli zao hizo unatia shaka kubwa. Kama ni kweli Marekani, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zinataka kuthibitisha kuwa zina nia njema na ya kweli, ziache kuendelea kuziuzia silaha Saudia na Imarati ili kuvunja nguvu na uwezo wa tawala hizo vamizi wa kuendeleza vita vya kidhalimu dhidi ya wananchi wa Yemen.

Hivi sasa, zaidi ya miaka mitano imepita tangu muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia na Imarati ulipoanzisha vita dhidi ya Yemen, lakini madola ya Magharibi yangali yanaendelea kuusaidia na kuunga mkono kikamilifu muungano huo vamizi kisilaha na kilojistiki. Hatua hiyo ya Marekani na nchi za Ulaya inayozingatia na kujali faida nono ya fedha, maslahi ya kiuchumi na ustawi wa sekta zao za viwanda vya silaha inayafanya madola hayo ya Magharibi yawe washirika kamili wa jinai zinazofanywa na muungano wa Saudia za mauaji ya wananchi madhulumu wa Yemen.../ 

Tags

Maoni