Oct 21, 2020 12:18 UTC
  •  Kikao cha Baraza la Usalama la UN kuhusu usalama wa Ghuba ya Uajemi

Eneo la Ghuba ya Uajemi ambalo ni miongoni mwa maeneo ya kistratijia ya dunia na yenye umuhimu mkubwa katika soko la kimataifa la masuala ya uchumi na nishati. Kwa kuzingatia uhakika huo usalama wa eneo hilo muhimu la majini daima umekuwa ukipewa mazingatio makubwa katika taasisi za Umoja wa Mataifa.

Katika mkondo huo Jumanne ya jana Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliitisha kikao kilichofanyika kwa njia ya video chini ya uenyekiti wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov. Akihutubia kikao hicho, Katibu Mkuu wa umoja huo, Antonio Guterres, ameyataja makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kuwa ni muhimu sana kwa ajili ya usalama wa Ghuba ya Uajemi. Guterres amesisitiza udharura wa kulindwa makubaliano hayo na kuongeza kuwa: "Suala la kuzuia silaha za nyuklia linapaswa kupewa umuhumi mkubwa zaidi na tangu hapo awali nilikuwa na imani kwamba mapatano ya JCPOA ni wenzo muhimu kwa ajili ya usalama wa Ghuba ya Uajemi."

Antonio Guterres

Sisitizo la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu udharura wa kulindwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na uhusiano wake wa moja kwa moja na usalama wa eneo la Ghuba ya Uajemi na amani na usalama wa eneo la Magharibi mwa Asia kwa ujumla, linadhihirisha msimamo wa taasisi hiyo ya kimataifa ambayo Baraza lake la Usalama ndilo lenye jukumu la kulinda usalama wa dunia mkabala wa msimamo wa Marekani unaopinga makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Si hayo tu bali Marekani pia inahatarisha usalama wa Ghuba ya Uajemi baada ya kutuma vikosi vya majeshi katika eneo hilo nyeti na la kistratijia. Ni kutokana na hali hiyo ndiyo maana Jamhuri ya Kiislamu inapinga kwa nguvu zote suala la kuwepo majeshi ya madola ajinabi katika eneo hilo na mwaka jana ilitoa pendekezo la kuanzishwa mfumo wa usalama utakaozishirikisha nchi zote za eneo hilo. Akihutubia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran, Muhammad Javad Zarif aliashiria mpango wa Tehran wa "Amani ya Hormuz" na kusema: "Msingi wa mpango na pendekezo hilo ni wajibu na jukumu la kila nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi katika kulinda usalama, amani na kudhamini hali bora ya nchi jirani na manufaa ya pande zote."

Muhammad Javad Zarif

Nukta nyingine yenye umuhimu ni kwamba wanachama wote wa kundi la 4+1 linalojumuisha nchi za Mashariki yaani Russia na China na zile za Magharibi ambazo ni Ujerumani, Ufaransa na Uingereza, na Umoja wa Ulaya kwa ujumla, zinaafikiana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres kuhusu umuhimu wa makubaliano ya JCPOA katika kulinda usalama na amani ya Ghuba ya Uajemi. Pande hizo zote zinaamini kuwa makubaliano hayo ya nyuklia ni mfano kamili wa mapatano ya kimataifa ya kulinda usalama wa kikanda na kimataifa. Hata hivyo na kinyume na matakwa ya jamii ya kimataifa, Rais Donald Trump wa Marekani mwezi Mei mwaka 2018 aliiondoa nchi hiyo katika makubaliano hayo muhimu yanayodhamini usalama wa kimataifa na kuanza kutekeleza vikwazo ambavyo havijawahi kushuhudiwa katika historia kwa ajili ya kuilazimisha Tehran isalimu amri kwa matakwa yake yasiyo ya kisheria. Hii ni licha ya kwamba Iran imetekeleza kikamilifu majukumu yake yote kwa mujibu wa makubaliano hayo ya JCPOA.

Baada ya kujiondoa katika mapatano ya JCPOA, serikali ya Trump imekuwa ikifanya mikakati ya kusambaratisha makubaliano hayo na daima imekuwa ikiwashinikiza waitifaki wake wa Ulaya ikiwataka wajiondoe katika makubaliano hayo na kuanzisha tena vikwazo vya kimataifa dhidi ya Iran. Hata hivyo sisitizo la mara kwa mara la maafisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Ulaya kuhusu ulazima wa kulindwa makubaliano hayo ni kielelezo cha mtazamo wao unaotofautiana na wa Marekani katika uwanja huo. Kwa sasa makubaliano hayo ya JCPOA ni miongoni mwa mambo yaliyozusha hitilafu kubwa baina ya pande hizo mbili za Bahari ya Atlantic. Mtaalamu wa masuala ya eneo la Asia Magharibi, Muhammad Afandi anasema: "Marekani daima imekuwa ikifanya mikakati ya kuibua migogoro na machafuko katika eneo la Magharibi mwa Asia kwa shabaha ya kupata soko la silaha; na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yanakinzana na sera hiyo ya Washington." 

Donald Trump

Wanachama wa Mashariki wa makubaliano hayo hususan Russia mbali na kusisitiza udharura wa kulindwa JCPOA wamekuwa wakitahadharisha kuhusu njama chafu za Marekani katika eneo la Ghuba ya Uajemi. Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergey Lavrov amekiambia kikao cha jana cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba: "Siasa za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za Marekani kuhusiana na eneo la Ghuba ya Uajemi zimefeli, na sera za kutoa vitisho dhidi ya nchi nyingine ni makosa na hatari." Lavrov alikuwa akiashiria vitisho vya Marekani dhidi ya Iran katika kipindi chote cha miaka miwili ya hivi karibuni kwa kisingizio cha kuweka mashinikizo ya kiwango cha juu na katika fremu hiyo imezidisha vikosi vya majeshi yake katika eneo la Ghuba ya Uajemi. 

Tags

Maoni