Oct 22, 2020 12:21 UTC
  • Wazayuni waliofilisika kwa corona waongezeka kwa asilimia 40

Kuenea maambukizi ya kirusi cha corona katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na ambazo zimepachikwa jina bandia la Israel, kumekuwa na madhara makubwa kwa uchumi wa utawala wa Kizayuni na sasa hivi Wazayuni waliofilisika kutokana na ugonjwa huo hatari wameongezeka kwa asilimia 40.

Mtandao wa Kizayuni wa "Walla" umechapisha ripoti leo Alkhamisi na kulinukuu Baraza la Mawaziri la utawala wa Kizayuni likisema kuwa, mwaka huu, mashirika 4,000 zaidi ya Israel yametangaza kufilisika ikilinganishwa na mwaka uliopita, na sababu yake ni madhara ya kuenea ugonjwa wa COVID-19 na karantini zilizowekwa.

Afisa mmoja wa utawala wa Kizayuni amenukuliwa na mtandao huo akisema kwamba hatua zilizochukuliwa kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa corona zimeleta madhara makubwa ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika sekta ya ajira ya utawala huo.

Takwimu za karibuni zinaonesha ongezeko kubwa la maambukizi ya corona ndani ya utawala wa Kizayuni na zaidi ya Wazayuni 307,765 wamethibitishwa kuambukizwa ugonjwa huo kwa mujibu wa ripoti za serikali ya Israel.

Vitongoji vya walowezi wa Kizayuni

 

Wakati huo huo serikali ya Qatar kwa mara nyingine imeutaka utawala wa Kizayuni uache kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi ulizowapora Wapalestina.

Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Qatar (QANA), jana usiku serikali ya Doha ilitoa taarifa na kutangaza kuwa, kuendelea ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, ni tishio na changamoto inayozikabili sheria na maazimio ya kimataifa hasa azimio nambari 2334 la Baraza la Usalama, na kutaka hatua za haraka za kimataifa zichukuliwe ili kuulazimisha utawala wa Kizayuni ukomeshe mara moja ujenzi wa vitongoji vya walowezi hao.

Tags

Maoni