Oct 23, 2020 07:49 UTC
  • Madai ya kukaririwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kinyume cha ukweli wa mambo

Anwar Gargash Waziri Mshauri wa Mambo ya Nje katika Umoja wa Falme za Kiarabu ametuma ujumbe kupitia ukurasa wake wa Twitter na kudai kuwa, Iran inavuruga uthabiti katika eneo la Asia Magharibi.

Gargash amedai kuwa: "Uangaziwaji mpya wa kihistoria na wa kimataifa kwa usalama wa eneo la Ghuba (ya Uajemi) unapaswa kuanza kwa kuaminiana. Haya ni mambo ambayo yamekumbwa na taathira hasi  katika miaka ya hivi karibuni kutokana na uingiliaji wa Iran katika mambo ya nchi za Kiarabu za Ghuba (ya Uajemi). Pasina kuwepo kuaminiana itakuwa vigumu kuelekea muundo mpya kwa ajili ya kuimarisha amani na uthabiti."

Hakuna shaka kuwa, kujenga hali ya kuaminiana ni sharti la kwanza la kuleta usalama katika eneo. Barry Buzan, mwananadharia wa uhusiano wa kimataifa anaamini kuwa, eneo la Ghuba ya Uajemi ni kati ya maeneo ambayo, yana mazingira bora ya kuunda muungano wa kiusalama kutokana na nukta kama vile, dini, lugha na jiografia. Muungano kama huo unaweza kubuniwa kutokana na nchi za eneo kuwa na maslahi ya pamoja kwa ajili ya kuleta usalama wa kieneo.

Pamoja na hayo, Ghuba ya Uajemi ni kati ya maeneo ambayo si tu kuwa hayana muungano wa kiusalama bali hata kundi dogo la usalama ambalo limeundwa na kupewa jina la Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi limefeli na kushindwa kufikia malengo yake. Kuna sababu kadhaa za kufeli huko na sababu kuu ni ukosefu wa kuaminiana baina ya nchi wanachama. Nukta muhimu hapa ni kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na sera zake si chanzo cha ukosefu wa kuaminiana katika eneo.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katu haijafuatilia sera za uvamizi katika eneo la Asia Magharibi bali imekuwa ikijihami yenyewe au waitifaki wake ili kuzuia hujuma.

Ghuba ya Uajemi

 

Uwepo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Syria ulikuwa na utambulisho wa kiulinzi pekee kwani Syria, ambayo ni muitifaki wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, iliomba msaada wa Iran katika kukabiliana na magaidi ambao wanaungwa mkono na Marekani, utawala wa Kizayuni na baadhi ya nchi za Kiarabu hasa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu. Ni wazi kuwa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu zimekuwa zikitekeleza sera haribifu katika eneo la Asia Magharibi ikiwa ni pamoja na kuivamia Yemen. Katika kipindi cha miaka sita tokea nchi hizo mbili za Kiarabu ziivamie Yemen, zimekuwa zikidondosha mabomu kila siku katika nchi hiyo na kuisababishia maafa ambayo ni makubwa zaidi duniani hivi sasa.

Nukta nyingine ni kuwa ukosefu wa usalama katika eneo la Asia Magharibi unatokana na ununuzi mkubwa wa silaha wa baadhi ya nchi za Kiarabu katika eneo. Aidha uwepo wa majeshi ya madola ya Magharibi, hasa Marekani, katika eneo kwa lengo la kuizingira Iran, unaweza kuwaletea usalama watawala wa baadhi ya nchi lakini kwa ujumla uwepo huo haujaweza kuleta usalama katika eneo. Uwepo huo wa majeshi ajinabi haujaweza kuleta usalama kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambayo ni dola muhimu na lenye nguvu kubwa katika eneo. Mfano wa wazi wa ukosefu wa amani ulioibuliwa na majeshi ajinabi katika eneo ni kuuawa kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na Abu Mahdi al Muhandes, Naibu Kamanda wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq, Al Hashd al Shaabi. Wawili hao na wenzao waliokuwa nao waliuawa shahidi mwezi Januari katika hujuma ya jeshi la Marekani mjini Baghdad. Mbali na hayo, wanajeshi wa Marekani ambao wako katika ardhi ya Iraq, wamekuwa wakitekeleza mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya harakati za muqawama katika eneo.

Meli ya kivita ya Marekani katika Ghuba ya Uajemi

Hakuna shaka kuwa, moja ya sababu nyingine za ukosefu wa usalama katika eneo la Asia Magharibi ni uwepo wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Mbali na kuwa Israel imeanzisha vita kadhaa vya kichokozi dhidi ya nchi za Kiarabu, lakini pia, kwa himaya ya Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya, imekalia kwa mabavu ardhi za Palestina. Hivi sasa Wapalestina wamebakia na chini ya asilimia 15 ya ardhi zao za asili. Kwa hivyo hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel si tu kuwa haitaleta amani katika eneo bali ni chanzo cha kuendelea ukosefu wa usalama kwa sababu Wapalestina sasa wataimarisha azma yao ya kukabiliana na jinai za utawala wa Kizayuni.

Nukta ya mwisho ni kuwa, kinyume na alivyodai Anwar Gargash, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaongoza katika kuchukua hatua za kujenga hali ya kuaminiana. Hii ni katika hali ambayo baadhi ya nchi za Kiarabu zimechukua muelekeo wa kikabila na kikaumu katika kudai kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haipaswi kujihusisha katika masuala ya nchi za Kiarabu. Nchi hizo za Kiarabu sasa zinajikurubisha kwa utawala wa Israel kwa lengo la kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na jambo hilo ni kizingiti kikubwa katika kuwepo hali ya kuaminiana katika eneo.

Tags

Maoni