Oct 23, 2020 08:03 UTC
  • Iraq: Baghdad inaunga mkono haki ya Wapalestina ya kujiamulia muskatabali wao

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq amekanusha habari za uvumi zinazodai kuwa Baghdad inataka kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusisitiza kuwa, taifa hilo linaunga mkono haki ya Wapalestina ya kujiamulia muskatabali wao wenyewe.

Fouad Hussein amesema msimamo na sera ya Iraq kuhusu taifa la Palestina iko wazi na wala haijabadilika.

Afisa huyo wa ngazi za juu wa Iraq amenukuliwa akisema hayo leo Ijumaa na kueleza bayana kuwa, "ukombozi wa wananchi madhulumu Wapalestina na kuundwa taifa huru la Palestina ni mambo ambayo daima yamekuwa yakiungwa mkono na taifa na serikali ya Iraq."

Kufuatia mapatano ziliyofanya Imarati na Bahrain ya kuanzisha uhusiano rasmi na utawala wa Kizayuni wa Israel mnamo Septemba 15, habari zilienea kuwa baadhi ya nchi za Kiarabu ziko mbioni kufuata mkumbo huo wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Tel Aviv.

Maandamano ya wananchi wa Bahrain ya kupinga kuanzishwa uhusiano na Israel

Kadhalika Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq amepuuzilia mbali uvumi kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo ya Kiarabu, Mustafa al-Kadhimi anapanga kuitembelea Syria.

Baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti katika siku chache zilizopita kuwa, kuna uwezekano Waziri Mkuu wa Iraq ataitembelea Syria.

Tags