Oct 24, 2020 02:36 UTC
  • Kurudi tena Saad Hariri; 'mwokozi' mkoroga jungu la migogoro ya ndani Lebanon

Kwa mara nyingine tena, Saad Hariri amekuwa Waziri Mkuu wa Lebanon baada ya bunge kumpigia kura ya kuwa na imani naye.

Kuna nukta kadhaa ambazo inafaa kuziashiria hapa kuhusiana na kuteuliwa Hariri na kupigiwa kura ya imani ya kumwezesha kuunda baraza la mawaziri.

Nukta ya kwanza ni kwamba, hii ni mara ya tatu ndani ya kipindi cha miaka minne ambapo Saad Hariri amekabidhiwa jukumu la kuunda serikali. Alifanya hivyo pia mwaka 2016 na 2018, lakini Oktoba 2019 alijiuzulu wadhifa wa uwaziri mkuu, siku 13 tu baada ya kuanza maandamano ya upinzani ya wananchi.

Nukta ya pili ni kuwa, kati ya wabunge 128 ni 65 tu ndio waliompigia Hariri kura ya kumuunga mkono, wakati Mustafa Adib, waziri mkuu mpendekezwa wa kabla yake alipata kura 90 za kuwa na imani naye. Kwa maneno mengine ni kwamba Saad Hariri ameweza kukamilisha ile idadi tu ya kura zilizohitajika ili kupata imani ya bunge la Lebanon. Sayyid Hadi Sayyid Afqahi, mtaalamu wa masuala ya Asia Magharibi anasema, Hariri amepungukiwa na kura 25 za kuwa na imani naye za bunge kulinganisha na Adib, wakati Adib hana umaarufu mkubwa wa kisiasa ndani ya nchi hiyo.

Saad Hariri

Nukta nyingine ya tatu ya kuashiria hapa ni kwamba, Hizbullah na Harakati Huru ya Kitaifa hazikumuunga mkono Saad Hariri awe waziri mkuu, lakini harakati ya Amal imefanya hivyo. Hata ndani ya Harakati ya Machi 14 pia kuna baadhi ya makundi ambayo yamepinga uwaziri mkuu wa Saad Hariri. Walid Junbalat, kiongozi wa chama cha Maendeleo ya Kisoshalisti na Samir Jaajaa, anayeongoza chama cha Makundi ya Kilebanon walitangaza tokea awali kuwa wanapinga Hariri kutawazwa kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo. Kwa muktadha huo ndiyo kusema kuwa Saad Hariri amekabidhiwa jukumu la kuunda serikali akiwa na uungaji mkono dhaifu.

Nukta ya nne ni kwamba, vyombo vya habari vilivyo karibu na Hariri vimemtangaza na kujaribu kumuonyesha yeye kuwa ni 'mwokozi' wa Lebanon. Kwa miaka minne sasa Lebanon imekuwa na mawaziri wakuu watatu ambao ni Saad Hariri, Hassan Diyab na Mustafa Adib. Baada ya Adib kushindwa kuunda serikali, endapo Hariri atafanikiwa kufanya hivyo, atakuwa Waziri Mkuu wa nne wa nchi hiyo ndani ya kipindi hiki cha miaka minne, ambapo yeye peke yake atakuwa ameshaunda baraza la mawaziri mara tatu.

Kuweka wazi zaidi nukta hii ni kwamba, kuanzia mwaka 2009 hadi 2011, ni Saad Hariri ndiye aliyekuwa Waziri Mkuu wa Lebanon. Na kwa maneno mengine ni kuwa, katika muda wa muongo mmoja sasa, yeye ameshikilia wadhifa huo mara tano. Kwa muktadha huo inafaa kujiuliza, vipi mtu ambaye amekalia kiti cha uwaziri mkuu mara nyingi zaidi kuliko mtu yeyote mwengine aje kuwa mwokozi wa kuivusha Lebanon na matatizo kadha wa kadha yanayoikabili katika nyuga mbali mbali? Kwa kweli hiyo ndiyo sababu kuu iliyoifanya Hizbullah na Harakati Huru ya Kitaifa zipinge Hariri kuwa waziri mkuu kwa sababu ndiye mkorogaji mkuu wa jungu la migororo ya ndani ya Lebanon.

Bunge la Lebanon

Nukta ya tano ni kuwa, baada ya Saad Hariri kupigiwa kura ya kuwa na imani naye na bunge alisema, ataunda serikali ya shakhsia wataalamu wasio wa kisiasa, ambayo itakuwa na jukumu la kuleta mageuzi ya kiuchumi na ya mfumo wa kifedha wa Lebanon. Aidha amedai kuwa, mirengo mikuu bungeni imeahidi kuiunga mkono serikali yake kwa ajili ya kutekeleza mageuzi hayo. Pamoja na hayo, utendaji wa Hariri, hasa katika mwaka 2018 umeonyesha kuwa, anaendesha mambo sana "kichama", kiasi kwamba hata makundi ya Masuni ambayo si wanachama wa harakati yake ya Machi 14 hayapi nafasi ya kuwa na sauti yoyote. Kwa sababu hiyo, ahadi yake ya kuunda serikali isiyo na utashi wa kichama ni propaganda tu ya kujitangaza kwenye vyombo vya habari.

Ama nukta ya sita na ya mwisho ni kuwa, Hariri anakabidhiwa jukumu la kuunda baraza la mawaziri kwa mara ya tatu ndani ya kipindi cha miaka minne, wakati, kwa kuzingatia kura 65 alizopigiwa na wabunge, serikali tarajiwa atakayounda itapitishwa kwa kura chache pia. Na kama atafanikiwa kuiunda, serikali hiyo itakabiliwa na changamoto kali zikiwemo za matatizo kadhaa ya kiuchumi, mripuko wa virusi vya corona na hitilafu kubwa za kisiasa za ndani ya Lebanon.../

Tags

Maoni