Oct 24, 2020 04:20 UTC
  • Hamas: Israel haiwezi kuvunja azma na mapambano ya Wapalestina

Msemaji wa Harakati ya Mapambabno ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema kuwa lengo la mashambulizi ya mara kwa mara ua utawala haramu wa Israel dhidi ya eneo la Ukanda wa Gaza ni kuvunja azma ya mapambano ya taifa la Palestina lakini utawala huo utashindwa na kugonga mwamba.

Hazem Qassem amelaani mashambulizi yaliyofanywa na ndege za kivita za Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza na kusema kuwa, viongozi wa utawala wa Kizayuni wanataka kusitisha vita na mapambano ya taifa la Palestina ya kukomboa ardhi iliyoghusubiwa kwa mashambulizi kama hayo.

Hazem Qassem amesisitiza kuwa Wapalestina watadumisha mapambano ya kukomboa nchi yao kutoka kwenye makucha ya Wazayuni maghasibu na kuongeza kuwa: Hatua ya hivi karibuni ya baadhi ya nchi za Kiarabu ya kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel imewahamasisha viongozi hao kufanya mashambulizi zaidi dhidi ya taifa la Palestina. 

Alfajiri ya Alkhamisi iliyopita, ndege za kivita za Israel zilishambulia kambi ya Arin ya Batalioni ya Izzuddin Qassam, tawi la kijeshi la harakati ya Hamas na kambi nyingine ya wanapambano wa Palestina huko Mashariki mwa mkoa wa Rafah katika Ukanda wa Gaza. 

Ndege hizo za Israel pia zilishambulia kwa mabomu mashamba ya kilimo ya kitongoji cha al Qararah huko Kaskazini Mashariki mwa mji wa Khan Yunis.    

Tags

Maoni