Oct 26, 2020 02:32 UTC
  • 'Mapatano ya Saudia na Israel itakuwa zawadi Aal Saud watakayomtunukia rais ajaye wa Marekani'

Mkuu wa shirika la ujasusi la utawala haramu wa Israel, Mossad amesema utawala wa Aal Saud unataka kumtunukia kama zawadi rais ajaye wa Marekani mapatano itakayofanya ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo wa Kizayuni.

Yossi Cohen ameongeza kuwa, kufikiwa mapatano na kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Saudi Arabia kutatangazwa baada ya kufanyika uchaguzi wa rais wa Marekani kwa sababu utawala wa Aal Saud ungependa mapatano utakayofanya na Israel yawe ni aina fulani ya hidaya na zawadi ya Saudia kwa rais ajaye wa Marekani.

Cohen amebainisha kuwa, makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida kati ya Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni yatashurutisha pia Marekani kuiuzia silaha Riyadh.

Yossi Cohen

Siku ya Ijumaa iliyopita ya tarehe 23 Oktoba Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuwa Sudan na Israel zimefikia mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida wa kidiplomasia, ikiwa na maana ya Sudan kujiunga na nchi zingine za Kiarabu na Kiislamu za Misri, Jordan, Imarati na Bahrain kuutambua rasmi utawala huo haramu wa Kizayuni unaoikalia kwa mabavu Palestina na Qud tukufu.

Kabla ya Sudan, tarehe 15 ya mwezi uliopita wa Septemba mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Bahrain walitia saini makubaliano ya kutangaza uhusiano wa kawaida baina ya nchi zao na utawala ghasibu wa Israel.

Makubaliano hayo yalisainiwa katika hafla iliyofanyika katika Ikulu ya Marekani, White House, na kuhudhuriwa na Rais wa Marekani, Donald Trump na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala dhalimu wa Israel.../

Tags