Oct 26, 2020 02:33 UTC
  • Maher al Akhras
    Maher al Akhras

Ripota wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zilizopewa jina la Israel ameutaka utawala wa Kizayuni umwachie Mpalestina Maher al Akhras haraka iwezekanavyo.

Kwa mujibu wa gazeti la Al-Qudsul-Araby, Michael Lynk, ripota wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Israel  amesema kuwaweka kizuizini Wapalestina ni ukiukaji wa wazi wa Makubaliano ya Nne ya Geneva na akasisitiza kuwa Israel inapaswa iyaheshimu makubaliano hayo.

Lynk ameongeza kuwa Tel Aviv inapaswa isitishe uwekaji kizuizini wa Wapalestina kwa kutumia kanuni ya kiidara na kuwaachia huru Wapalestina zaidi ya 350 ambao imewatia nguvuni na kuwaweka kizuizini kwa kutumia kanuni hiyo.

Michael Lynk

Maher al Akhras, Mpalestina mwenye umri wa miaka 49, mkazi wa mji wa Jenin katika eneo la Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan alikamatwa tarehe 27 Julai na kuwekwa kizuizini bila kuelezwa anakabiliwa na mashtaka gani.

Al Akhras amesusia kula chakula kwa muda wa siku 90 sasa kulalamikia kuwekwa kizuizini yeye mwenyewe pamoja na mateka wengine kadhaa wa Kipalestina waliokamatwa na mamlaka za utawala haramu wa Kizayuni na kuwekwa kizuizini kwa kutumia kanuni hiyo ya kiidara.

Kwa kuzingatia hali hiyo, mateka wengine 30 wa Kipalestina katika gereza ya Ofer, ambao ni wanachama wa Harakati ya Jihad Islami, Harakati ya Wananchi kwa ajili ya Ukombozi wa Palestina na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, wameamua kususia chakula katika kumuunga mkono Maher al Akhras.

Karibu mateka 4,800 wa Palestina wakiwemo wanawake 41 na watoto 140 wanashikiliwa katika jela za kuogofya za utawala wa Kizayuni wa Israel. Mateka hao wa Palestina ni miongoni mwa waathirika wakubwa wa jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel.../

 

Tags

Maoni