Oct 29, 2020 06:49 UTC
  • Kukwama mazungumzo ya amani ya Afghanistan; Trump apoteza karata ya turufu kabla ya uchaguzi wa rais

Serikali ya Afghanistan na kundi la Taliban ambazo tangu tarehe 12 mwezi Septemba zilianza mazungumzo ya amani huko Doha mji mkuu wa Qatar hadi sasa zimeshindwa kufikia mapatano. Kuhusiana na suala hilo, Zalmay Khalilzad Mjumbe Maalumu wa Marekani katika Masuala ya Afghanistan ambaye kwa mara kadhaa alikwenda Qatar kunakofanyika mazungumzo hayo ya amani amekiri waziwazi kwamba mazungumzo ya amani ya Afghanistan yamefeli.

Khalilzad amekiri kufeli mazungumzo ya amani ya Afghanistan katika hali ambayo licha ya timu za mazungumzo za serikali ya Afghanistan na kundi la Taliban kuwepo Qatar kwa muda wa mwezi mmoja na nusu lakini pande mbili hizo bado hazijakubaliana kuhusu ajenda ya mazungumzo yenyewewe, na wawakilishi wanne wa timu ya serikali pia wamerejea Kabul. Nukta kadhaa zinaweza kutajwa hapa kuhusu sababu za kushindwa mazungumzo  ya amani ya Afghanistan na taathira zake.   

Nukta ya kwanza ni kwamba, wajumbe wa kundi la Taliban na serikali ya Afghanistan wapo Qatar tangu tarehe 12 Septemba kwa lengo la kuhitimisha vita nchini Afghanistan; hata hivyo pande mbili hizo bado hazijaanza rasmi mazungumzo, na mashauriano kwa ajili ya kuanisha ajenda ya mazungumzo yenyewe pia yameshindwa kuzaa matunda. 

Nukta ya pili ni kuwa, lengo la mazungumzo ya amani ya Afghanistan lilikuwa kurejesha amani na utulivu katika jamii illiyokumbwa na vita ya Afghanistan; lakini inasikitisha kwamba sambamba na mazungumzo hayo ya Doha vita vimeongezeka katika aghalabu ya maeneo ya Afghanistan na waathirika wakuu ni raia wa kawaida. Yousef Al-Othaimeen, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ameeleza kusikitishwa na ongezeko la machafuko katika siku za hivi karibuni huko Afghanistan na kusisitiza kuwa, njia pekee ya kurejesha amani na utulivu nchini humo ni kutekelezwa usitishaji vita na kufanya mazungumzo haraka iwezekanavyo.  

Nukta inayofuata ni kwamba, kuongezeka machafuko na ukosefu wa amani nchini Afghanistan sambamba na kugonga mwamba mazungumzo ya amani baina ya serikali ya kabul na kundi la Taliban kumewafanya wananchi wa Afghanistan wapoteze imani kwa mazungumzo hayo. Waafghani hawana tena imani na mazungumzo hayo na baadhi ya weledi wa mambo wanaamini kuwa viongozi wa Marekani wanafanya jitihada  za kulidhihirisha kundi la Taliban na hata serikali ya Kabul kuwa ndio sababu ya kuendelea vita nchini humo kutokana siasa za undumakuwili Washington katika mchakato wa amani wa Afghanistan. Siasa hizo za Washington zina lengo la kuzipotosha fikra za walimwengu kuhusu chanzo halisi cha machafuko ambacho ni uwepo wa wanajeshi vamizi wa Marekani katika ardhi ya Afghanistan. 

Donald Trump

Nukta nyingine ni kuwa siasa za undumakuwili za Marekani zinakwamisha mafanikio ya mazungumzo ya amani ya Afghanistan kwa sababu Washington kwa upande mmoja inasisitiza udharura wa kufanyika mazungumzo hayo; na kwa upande wa pili inachukua hatua za kuzusha mtafaruku na hitilafu baina ya serikali ya Kabul na kundi la Taliban.

Tukiachilia mbali misimamo ya kindumakuwili ya Marekani kuhusiana na mazungumzo ya amani ya Afghanistan tunaona kuwa, wachambuzi wengi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa misimamo mikali na isiyolegeza kamba ya kundi la Taliban katika kipindi chote cha mazungumzo ya awali ya Doha ni miongoni mwa sababu za kushindwa mazungumzo hayoa. Kwa maneno mengine ni kuwa, msimamo wa kutaka kupata kila kitu wa timu ya kundi hilo katika mazungumzo ya Doha imekuwa sababu ya kushindwa kufikia mapatano baina ya pande mbili.

Mazungumzo ya Taliban na serikali ya Afghanistan

Mwisho kabisa inatupasa kusema kuwa, uchaguzi wa Rais wa Marekani unafanyika rasmi Jumanne ijayo wakati juhudi za Rais Donald Trump za kutaka kutumia mchakato wa mazungumzo ya amani ya Afghanistan kama turufu ya kampeni za uchaguzi huo ili kuzidisha nafasi ya kushinda uchaguzi, zikiwa zimegonga mwamba na kushindwa. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema Trump alikusudia kudhihirisha mapatano ya kisiasa baina ya serikali ya Afghanistan na kundi la Taliban kama mafanikio makubwa katika siasa zake za nje na kutumia suala la kukomesha vita vya muda mrefu zaidi katika historia ya Marekani kwa ajili ya kuzidisha kura zake katika uchaguzi ujao wa rais. Mwandishi wa gazeti la Washington Post mjini Kabul, Sayyid Salahuddin anasema: "Uchaguzi wa rais wa Marekani unafanyika wiki ijayo lakini hadi sasa hakuna mafanikio hata kidogo katika mchakato wa mazunguzo ya amani ya Afghanistan. Timu ya Trump ingeweza kutumia mapatano ya Waafghani kama karata ya tufuku kwenye uchaguzi wa rais na kuzidisha nafasi ya kuibuka na ushindi."

Zalmay Khalilzad na Donald Trump

Kwa ujumla inatupasa kusema kuwa, mazungumzo na Kiongozi wa Korea Kaskazini, kuzidisha mashinikizo dhidi ya China na Iran na hatimaye mazungumzo na kundi la Taliban vikuwa miongoni mwa maudhui kuu za siasa za kigeni za Donald Trump, na kiongozi huyo alikusudia kutumia masuala hayo kama karata ya turufu kwenye kampeni zake za uchaguzi wa rais. Hata hivyo jambo lenye uhakika ni kwamba, Trump anaingia mikono mitupu katika uchaguzi huo uliopangwa kufanyika tarehe 3 mwezi ujao wa Novemba.      

Maoni