Oct 30, 2020 07:27 UTC
  • Mauaji ya kigaidi ya viongozi; mbinu ya Kizayuni inayotumiwa na Saudi Arabia nchini Yemen

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Yemen imetangaza kupitia taarifa kwamba mashirika ya ujasusi ya nchi zinazounda muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia ndiyo yaliyopanga mauaji ya kigaidi ya Hassan Muhammad Zaid, Waziri wa Michezo na Vijana wa serikali ya uokovu wa kitaifa ya Yemen.

Hassan Zaidi, Waziri wa Michezo na Vijana wa serikali ya uokovu wa kitaifa ya Yemen, aliuliwa kigaidi siku ya Jumanne ya tarehe 27 Oktoba katika mji mkuu wa nchi hiyo Sana'a. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Yemen, Abdul Khaliq al-Ajri alitangaza siku ya Jumatano kwamba, mmoja wa waliohusika na mauaji hayo alikamatwa baada ya kujeruhiwa, lakini muuaji mwingine aliuawa baada ya kujaribu kukabiliana na vikosi vya usalama. Jana Alkhamisi, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Yemen ilitangaza katika taarifa nyingine kuwa, mashirika ya ujasusi ya muungano wa Saudia ndiyo yaliyoratibu shambulio hilo la kigaidi.

Abdul Khaliq al-Ajri

Ukifuatilia matukio ya Yemen utabaini kuwa, Saudi Arabia inatumia mauaji ya viongozi na maafisa wa Yemen, kama mbinu iliyoratibiwa na yenye shabaha maalumu, katika ilivyoanzisha dhidi ya nchi hiyo. Kitambo nyuma, utawala wa Riyadh ulitoa orodha ya watu 40 wenye mfungamano na Harakati ya Ansarullah na kutangaza kuwa, itampatia bakhshishi mtu yeyote atakayetoa taarifa kuhusu watu hao. Hassan Muhammad Zaid, Waziri wa Michezo na Vijana wa serikali ya uokovu wa kitaifa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Haki ni mmoja wa waliokuwemo kwenye orodha ya watu hao, ambao Saudia ilikuwa imepanga kuwaua.

Ukweli ni kwamba Saudia inayatumia mauaji ya kigaidi kama moja ya mbinu za kivita. Rashid al Haddad, mwandishi wa Kiarabu anaitakidi kuwa, utawala wa Aal Saud unatumia "mkakati wa pochi la fedha" kwa ajili ya kuwaua viongozi wa Yemen. Kulingana na mkakati huo, mashirika ya ujasusi ya Saudi Arabia yanawakodi baadhi ya watu na kuwaahidi kuwapatia fedha, kisha kuwatumia kutekeleza operesheni za mauaji.

Shahidi Hassan Muhammad Zaid

Sababu kuu iliyoifanya Saudia iamue kuwaua viongozi wa Yemen ni kwamba, utawala wa Aal Saud haukutarajia kama vita ulivyoanzisha dhidi ya nchi dhaifu zaidi na masikini zaidi ya Kiarabu katika eneo la Asia Magharibi vitaweza kuchukua muda wa takriban miaka sita. Si tu Aal Saud hawajaweza hadi sasa kushinda vita hivyo, lakini pia wanashuhudia majeshi yao na ya waitifaki wao yanavyoendelea kupata vipigo vikali kutoka kwa jeshi na vikosi vya kujitolea vya kamati za wananchi wa Yemen. Kwa hiyo utawala wa Riyadh umeamua kutumia mbinu ya mauaji ya kigaidi ili kujaribu kuwafuta shakhsia muhimu wenye vipawa wa serikali ya uokovu wa kitaifa ya Yemen.

Kabla ya hapo, Saleh As-Sammad, aliyekuwa Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen na Ibrahim Badruddin al-Houthi, ndugu wa Abdulmalik al-Houthi, Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah walikuwa miongoni mwa shakhsia muhimu waliouliwa shahidi na utawala wa Aal Saud. Turki al Maliki, msemaji wa muungano vamizi wa kijeshi wa Saudia alithibitisha kuwa, Ibrahim al Houthi aliuliwa kigaidi na muungano huo, lakini baada ya kupita siku chache muungano vamizi wa kijeshi wa Saudia ulikanusha kuhusika na mauaji hayo ili kujiepusha na ulipizaji kisasi wa jeshi na vikosi vya wananchi wa Yemen.

Shahidi Saleh As-Sammad

Mauaji ya kigaidi ya viongozi wa Yemen yanayofanywa na Saudi Arabia ni mbinu ambayo imekuwa ikitumiwa pia na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel dhidi ya makundi ya muqawama ya Palestina na Lebanon. Utawala wa kigaidi wa Israel nao pia umewaua shahidi viongozi wakuu kadhaa wa makundi ya muqawama ili kutoa pigo kwa muqawama wa Lebanon na Palestina.

Nukta nyingine kuhusiana na suala hili ni kasi ya uchukuaji hatua iliyoonyeshwa na vyombo vya usalama na intelijensia vya Yemen katika kuwatambua waliohusika na mauaji ya kigaidi ya Hassan Zaid. Baada ya kupita masaa 24 tu tangu lilipofanywa shambulio hilo la kigaidi, wahusika wa mauaji hayo walitambuliwa katika mkoa wa Dhamar; na hayo ni mafanikio muhimu kwa serikali ya uokovu wa kitaifa ya Yemen. Kuhusiana na suala hilo, Mahdi al Mashat, Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa na Kamanda Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Yemen amepongeza mafanikio makubwa ya vyombo vya intelijensia na usalama vya nchi hiyo kwa kuwatambua na kuwaangamizia waliomuua kigaidi Hassan Zaid akisisitiza kuwa hayo ni mafanikio muhimu kwa Yemen.../

Tags

Maoni