Nov 08, 2020 02:36 UTC
  • Sheria za Kiislamu zawekwa kando UAE baada ya kuanzishwa uhusiano na Israel

Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), umetangaza mabadiliko makubwa ya sheria za Kiislamu zinazohusu mtu binafsi ikiwemo kuruhusu watu ambao hawajaoana kuishi pamoja kiunyumba, kulegeza mipaka ya utumiaji pombe na kuyatambua "mauaji ya kulinda heshima" kuwa ni kosa la jinai.

Serikali ya Imarati imesema, mabadiliko hayo ya sheria ni sehemu ya juhudi za kuboresha mfumo wa sheria wa nchi hiyo na kustawisha mazingira ya uwekezaji na vilevile kuimarisha zaidi kile kinachotajwa kama "misingi ya kuvumiliana".

Tangazo la serikali ya Imarati la kulegeza utekelezaji wa sheria za Kiislamu zinazohusiana na masuala ya mtu binafsi limetolewa kufuatia hatua ya nchi hiyo pia ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, ambapo imeelezwa kwamba hatua ya kulegeza utekelezaji wa sheria hizo utapalekea nchi hiyo kutembelewa na watalii wengi na wawekezaji kutoka Israel.

Miongoni mwa mabadiliko yaliyofanywa katika sheria ya vileo, ni kufutwa adhabu iliyokuwa imewekwa kwa unywaji, uuzaji na umiliki wa pombe. Awali watu binafsi walilazimika kuwa ni kibali cha kuuza, kusafirisha na kuweka pombe majumbani mwao. Mabadiliko ya sheria hiyo yatawaruhusu hata Waislamu ambao walikuwa hawapatiwi vibali hivyo, kuweza sasa kunywa pombe bila kizuizi chochote katika nchi hiyo ya Kiislamu.

Hatua ya Imarati, pamoja na Bahrain na Sudan ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel imelaaniwa na kukosolewa vikali katika Ulimwengu wa Kiislamu na kutajwa kuwa ni uhaini na usaliti kwa malengo matukufu ya Wapalestina…/

 

Tags