Nov 11, 2020 14:46 UTC
  • Assad: Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi zinawazuia wakimbizi wasirudi Syria

Rais Bashar al Assad wa Syria amesema Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi zinawazuia wakimbizi wa Syria wasirudi nchini kwao.

Rais wa Syria ameyasema hayo leo katika mkutano wa kimataifa kuhusu kurejea wakimbizi wa Syria nchini mwao uliofanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo Damascus. Assad ameeleza kwamba, baadhi ya nchi za Magharibi zinawatumia wakimbizi kwa matashi ya kisiasa.

Rais Bashar al Assad amesema, nchi hizo za Magharibi zinatumia mbinu ya kutoa vitisho na kurubuni ili kuwazuia wakimbizi Wasyria wasirudi makwao na akabainisha kuwa, serikali ya Damascus inafanya kila juhudi kwa ajili ya kuwarejesha wakimbizi wote Wasyria nchini humo lakini juhudi hizo zinakabiliwa na vizuizi kadhaa.

Mbali na kueleza kwamba akthari ya Wasyria walioko nje ya nchi wana hamu ya kurejea nchini kwao, Rais wa Syria amezishukuru pia nchi zilizowapokea wakimbizi hao na vilevile misaada iliyotolewa na Iran na Russia kwa ajili ya kupunguza athari za vita na mzingiro iliowekewa Syria, pamoja na jitihada zao za kuwezesha kufanyika mkutano huo wa kimataifa wa Damascus wa wakimbizi Wasyria kurudi nchini kwao.

Wakimbizi wa Syria

Vita vilivyoanzishwa na magenge ya kigaidi dhidi ya Syria kwa msaada wa nchi za eneo na baadhi ya madola ya Magharibi vilisababisha mamilioni ya Wasyria kuyahama makazi yao na kukimbilia maeneo ya usalama ndani na nje ya nchi hiyo katika nchi jirani za Uturuki, Lebanon na Jordan.

Leo mji mkuu wa Syria, Damascus ni mwenyeji wa mkutano wa kimataifa wa "Wakimbizi wa Syria" ambao unahudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi za China, Russia, Iran, Lebanon, Imarati, Pakistan na Oman.

Ajenda za mkutano huo wa siku mbili ni kujadili namna ya kurahisisha njia za kuwawezesha wakimbizi Wasyria warejee nchini mwao kwa kutilia maanani janga la maambukizi ya virusi vya corona na vile vile vikwazo vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya Syria.

Inakadiriwa kuwa kati ya watu wote milioni 17, Wasyria wapatao milioni tano na laki tano wanaishi ukimbizini nje ya nchi na wengine wapatao milioni sita ni wakimbizi wa ndani ya nchi walioyahama makazi yao.../

Tags