Nov 17, 2020 03:52 UTC
  • Tuhuma za kutumika ardhi ya Afghanistan katika kushambuliwa nchi nyingine zakanushwa

Serikali ya Afghanistan imekanusha tuhuma za kutumika ardhi ya nchi hiyo kufanya mashambulizi dhidi ya nchi nyingine.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Afghanistan imepinga madai ya viongozi wa Pakistan kwamba ardhi ya nchi hiyo inatumiwa na magaidi na maafisa wa intelijensia  wa India kufanya mashambulio dhidi ya nchi hiyo.

Wizara hiyo imesisitiza azma ya Afghanistan ya kuendelea kupambana na ugaidi na kuongeza kwamba serikali ya Kabul haitaruhusu magaidi kutumia ardhi yake kushambulia nchi nyingine.

Shah Mahmoud Quraishi, Waziri wa Mambo ya Nje na Babar Iftikhar, msemaji wa jeshi la Pakistan hivi karibuni wamenukuliwa wakisema kuwa majasusi wa India wamekuwa wakitumia ardhi ya Afghanistan kupanga mipango ya kuishambulia kiintelijensia Pakistan.

Viongozi wa Kabul na Islamabad wamekuwa wakituhumiana kwamba wanaruhusu magaidi au maafisa wa ujasusi wa nchi nyingine kutumia ardhi zao kwa ajili ya kufanya mashambulizi dhidi ya upande wa pili.

Shah Mahmoud Quraishi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan

Tuhuma kwamba Afghanistan inaruhusu ardhi yake kutumiwa na majasusi na maafisa wa usalama wa India kwa ajili ya kutoa pigo dhidi ya Pakistan zinatolewa na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo katika hali ambayo serikali ya Kabul inajitayarisha kumkaribisha nchini Afghanistan Imran Khan, Waziri Mkuu wa Pakistan kwa lengo la kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo kuhusu njia za kuimarisha uhusiano wa pande mbili na vile vile kujadili masuala ya mazungumzo ya amani na kundi la Taliban.

Katika miaka ya karibuni Afghanistna na Pakistan zimekuwa zikituhumiana kuhusu mambo mbalimbali na hasa ya kiusalama, jambo ambalo limeacha taathira hasi katika uhusiano wa nchi hizo jirani.

Viongozi wa Pakistan wanaituhumu Afghanistan kuwa inaruhusu ardhi yake kutumiwa na majasusi pamoja na maafisa wa usalama wa India kuendesha vita vya intelijensia dhidi ya maslahi yake ya kitaifa, tuhuma ambazo zimekuwa zikikanushwa mara kwa mara na viongozi wa Kabul.

Rajah Majid Javid Ali Behti, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Pakistan anasema:  Shirika la Intelijensia la India, RAW, na Idara ya Usalama ya Afghanistan zinahusika katika machafuko ya jimbo la Baluchestan kwa lengo la kuidhoofisha serikali ya Islamabad.

Serikali ya Afghanistan nayo inaituhumu Pakistan kuwa imegeuka kuwa maficho salama kwa magaidi ambao wanashirikiana na serikali ya Islamabad kuendesha vita dhidi ya nchi hiyo.

Kwa kuzingatia wingu zito la shaka na dhana mbaya ambalo limekuwa likitawala kwa miaka mingi uhusiano wa nchi mbili jirani za Pakistan na Afghanistan, mashauriano na safari ambazo zimekuwa zikifanywa na viongozi wa kisiasa na kiusalama wa nchi mbili katika miji mikuu ya nchi hizo, hazijasaidia lolote katika kupunguza hitilafu na mivutano iliyopo.

Magaidi wa Taliban

Kutokuwa na taathira kubwa safari za viongozi wa nchi hizo katika miji mikuu ya pande mbili na hasa katika muongo uliopita katika kupunguza hitilafu na kuimarisha ushirikiano, kumefanya safari inayotazamiwa kufanywa wiki hii na Imran Khan, Waziri Mkuu wa Pakistan huko Kabul kutotoa matumaini yoyote ya kufikiwa natija ya kuridhisha.

Ni kwa msingi huo ndipo safari na mashauriano ya viongozi wa nchi hizo yakachukuliwa kuwa ya kimaonyesha tu yanayokusudiwa kuwaridhisha raia wa nchi hizo na kuwaonyesha kwamba viongozi wao wanafanya juhudi za kuboresha uhusiano wa pande mbili.

Hii ni katika hali ambayo watu wa Afghanistan na Pakistan wanafahamu vyema kwamba kuna mvutano mkubwa kati ya nchi hizo na kwamba safari za hivi sasa za viongozi wa Islamabad na Kabul, hazitasaidia pakubwa katika kutatua matatizo yaliyopo.

Tags