Nov 21, 2020 02:34 UTC
  • Utayari wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina wa kuzungumza na kushirikiana na Israel

Mohammad Shtayyeh, Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa mamlaka hiyo uko tayari kuanzisha tena mazungumzo na ushirikiano wa masuala ya usalama na utawala haramu wa Israel.

Kabla ya hapo Hussein as-Sheikh, Msimamizi wa Wizara ya Masuala ya Kiraia wa mamlaka hiyo alikuwa tayari ameashiria utayari wa mamlaka hiyo wa kuanzisha tena ushirikiano wa masuala ya usalama kati ya pande mbili hizo.

Uhusiano wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na makundi ya mapambano ya Kipalestina yamekuwa yakiathiriwa na masuala kadhaa katika miezi ya karibuni. Tarehe 28 Januari mwaka huu Rais Donald Trump wa Marekani alizindua mpango wa kibaguzi alioupa jina la Mauamala wa Karne na nchi tatu za Kiarabu za Bahrain, Imarati na Oman ambapo Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel pia alishiriki.

Suala jingine ni tangazo la Israel la kuunganisha sehemu ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo wa Kizayuni. Kufuatia tangazo hilo, tarehe 19 Mei mwaka huu, Mamlaka ya Ndani ya Palestina ilichukua uamuzi wa kusimamisha ushirikiana na mazungumzo yote na utawala huo.

Suala jingine ambalo limeathiri uhusiano wa Wapalestina na utawala wa Israel ni uamuzi wa nchi tatu za Kiarabu za Bahrain, Imarati na Sudan kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala huo. Uamuzi huo uliwapelekea Wapalestina kufikia natija hii kwamba ili kudhamini maslahi yao ya kitaifa wanapasa kutoitegemea nchi yoyote ile bali ni wao wenyewe ndio wanapasa kutatua masuala yao ya ndani na kuimarisha umoja wao wa kitaifa, ili kujilinda mbele ya hujuma ya utawala wa Kizayuni.

Mohammad Shtayyeh

Katika hali ambayo mazungumzo ya kuimarisha ushirikiano na umoja wa kitaifa baina ya makundi tofauti ya Kipalestina yalikuwa yanaendelea vizuri katika miji ya Beirut na Istanbul, nayo Misri ambayo ni makao ya makundi kadhaa ya Palestina kutangaza habari ya kuyakutanisha makundi hayo, mwanzoni mwa wiki hii, na mara tu baada ya kutangazwa habari ya makundi hayo kuamua kuimarisha umoja wao wa kitaifa, ghafla Mamlaka ya Ndani ya Palestina ilitangaza uamuazi wake wa kuanzisha tena mazungumzo na ushirikiano na utawala wa Kizayuni kuhusu masuala ya usalama.

Swali muhimu hapa ni kwamba je, ni kwa nini mamlaka hiyo imepuuza uamuazi wa Wapalestina wa kuimarisha umoja wao wa kitaifa na kuamua kuanzisha tena mazungumzo hayo na utawala haramu wa Israel?

Kwa kutilia maanani kwamba Mamlaka ya Ndani ya Palestina ilikuwa ikishiriki vilivyo katika mazungumzo ya Cairo, ni wazi kuwa wakilishi wa mamlaka hiyo katika mazungumzo hayo walipewa habari ya kuwasaliti wenzao na makachero wa utawala wa Tel Aviv.

Katika upande wa pili, Mamlaka ya Ndani ya Palestina inautegemea pakubwa utawala wa Kizayuni kuhusua masuala ya uchumi na hasa kwa kutilia maanani kuwa kodi na ushuru unaotozwa maeneo ya wakazi wa Palestina yanayodhibitiwa na utawala wa Tel Aviv huwekwa moja kwa moja katika akaunti za utawala huo na kisha kuikabidha mamlaka hiyo kila mwezi. Kwa kuzingatia suala hilo, ni wazi kuwa utawala huo umetumia fedha hizo kama chombo cha kutoa mashinikizo dhidi ya Mamlakaya Ndani ili ikubaliane na matakwa yake.

Suala jingine mujimu ni kuhusu maafisa wa mamlaka hiyo. Mamlaka hiyo ina wafanyakazi na maafisa ambao hawaamini kuwa mapambano ndiyo njia bora zaidi ya kuushinikiza utawala wa Israel, na kwa msingi huo licha ya kuwepo ukatili na unyama wa kutisha unaofanywa na utawala huo dhidi ya Wapalestina, lakini maafisa hao hawako tayari kukabiliana nao bali wanasisitiza tu juu ya kuendelea kufanya mazungumzo yasiyo na faida yoyote na utawala huo. Ni wazi kuwa maafisa kama hao hawawezi kutegemewa hata kidogo katika kutetea maslahi ya kitaifa ya Palestina, bali ni mapambano tu ndiyo yanaweza kuwafanya Wapalestina wafikie malengo yao matukufu ya kitaifa.

Ukandamizaji wa Wazayuni dhidi ya Wapalestina

Suala jingine muhimu ni kwamba uamuzi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina wa kuanzisha tena mazungumzo ya ushirikiano na utawala wa kibaguzi wa Israel hautakuwa na natija nyingine ghairi ya kuzidisha hitilafu za ndani kati ya makundi ya Palestina na hivyo kuhatarisha zaidi maisha ya Wapalestina ambao wanaweza kulengwa wakati wowote na maghasibu wa Kizayuni. Suala hilo bila shaka litapunguza makali ya upinzani wa nchi za Kiislamu na makundi ya Palestina dhidi ya suala la nchi kadhaa saliti za Kiarabu kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Israel na wakati huohuo kuupa utawala huo fursa nzuri ya kuwachinja Wapalestina bila huruma wala kuogopa lolote.

Ni kwa msingi huo, ndipo uamuzi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina wa kuanzisha mazungumzo hayo na utawala wa Israel ukakabiliwa na ukosoaji mkubwa wa makundi ya mapambano ya Palestina. Ahmad Yusuf, mwanachama wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amekosoa vikali uamuazi wa mamlaka hiyo wa kuanzisha tena mazungumzo ya ushirikiano na utawala wa Kizayuni na kusisitiza kuwa mamlaka hiyo haina nia ya kweli ya kufuatilia maslahi ya makundi tofauti ya Palestina. Amesema wakati makundi hayo yalikuwa yamekutana mjini Cairo kwa ajili ya kufuatilia maslahi ya umoja wa taifa la Palestina na kuondoa tofauti zilizopo baina yao, habari ya kuanzishwa tena mazungumzo ya taratibu za kiusalama kati ya mamlaka hiyo na utawala ghasibu wa Israel ilikuwa dhoruba kali kwa Wapalestina.

Tags