Nov 22, 2020 04:12 UTC
  • Ubalozi wa Marekani Iraq ndio pekee duniani unaolindwa kwa mtambo wa makombora ya ulinzi wa anga

Mbunge wa mrengo wa As-Sadiqun katika bunge la Iraq amesema, ubalozi wa Marekani nchini humo ndio ubalozi pekee duniani unaolindwa kwa mtambo wa makombora ya ulinzi wa anga.

Kwa mujibu wa kituo cha habari cha Al-Ma'lumah, Ahmad al-Kanani amesema, hakuna ubalozi wowote duniani unaolindwa kwa kutumia mtambo wa makombora ya ulinzi wa anga, ndege za kivita na vifaru; kwa hiyo hatua hizo zinazochukuliwa na Marekani kwa ajili ya kulinda ubalozi wake wa mjini Baghdad zinakiuka sheria za kimataifa na mamlaka ya kujitawala ya Iraq.

Mnamo tarehe 4 Julai mwaka huu, kwa mara ya kwanza jeshi la Marekani liliufanyia majaribio mtambo wa ulinzi wa makombora aina ya Patriot katika ubalozi wake ulioko Baghda katika eneo la kijani lenye ulinzi wa hali ya juu. Eneo hilo la ubalozi wa Marekani lenya ukubwa wa hekta 42 ni kubwa zaidi kuliko hata mji wa Vatican.

Mbunge huyo wa Iraq wa mrengo wa As-Sadiqun amezungumzia pia kuondoka baadhi ya askari wa Marekani nchini Iraq na akasema, bunge la nchi hiyo lina mpango wa kuichukulia hatua Marekani na kwamba kuondoka askari hao hakutoshi.

Askari wa jeshi la kigaidi la Marekani wakiranda katika vichochoro vya mitaa ya Iraq

Mbunge mwingine wa Iraq Fadhil Jabir amesema, uamuzi wa kuondoka baadhi tu ya askari wa Marekani nchini Iraq ni operesheni ya "hadaa", kwa sababu kama Marekani ina nia ya kweli ya kuwaondoa askari wake nchini Iraq inapaswa kuainisha ratiba maalumu ya muda wa kuondoka askari hao katika makubaliano yake na serikali ya nchi hiyo na kulitangaza suala hilo katika vyombo vya habari.

Siku ya Jumanne iliyopita Kaimu Waziri wa Ulinzi wa Marekani Christopher Miller alitangaza kuwa, baadhi ya askari wa Marekani wataondoka katika ardhi ya Iraq na Afghanistan na kwamba idadi ya askari hao walioko Iraq itapunguzwa kutoka 3,200 hadi 2,500.../ 

Tags