Nov 22, 2020 12:29 UTC
  • Kambi ya kukabiliana na usaliti wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel yaasisiwa Lebanon

Shakhsia kadhaa wa Kiislamu, kisiasa na wa vyombo vya habari nchini Lebanon wametangaza kuwa wameanzisha kambi ya kukabiliana na hatua ya kihaini ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Toleo la leo la gazeti la al-'Ahd limeripoti kuwa, shakhsia hao wa Lebanon wametangaza kuwa, watateua jumbe kadhaa kutoka makundi tofauti ya Kiislamu kwa lengo la kuzielimisha na kuzitanabahisha nchi zingine kuhusu hatari ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni na matokeo mabaya ya kutekeleza mpango wa "Muamala wa Karne".

Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti hilo, katika safari iliyofanywa hivi karibuni na ujumbe wa harakati ya Palestina ya Hamas nchini Lebanon ujumbe huo ulikutana na viongozi wakuu kadhaa wa kisiasa wa nchi hiyo na kusisitizia ulazima wa kuchukuliwa hatua zaidi za kukabiliana na mwenendo wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni.

Baada ya Imarati na Bahrain kutangaza kuwa zimeafiki kuutambua rasmi utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, mnamo tarehe 15 Septemba, nchi hizo mbili za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi zilisaini rasmi mkataba wa kuanzisha uhusiano wa kawaida wa kidiplomasia na utawala huo unaoikalia Quds tukufu kwa mabavu, katika hafla iliyofanyika Ikulu ya White House, mjini Washington na kuhudhuriwa na rais Donald Trump wa Marekani na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Hafla ya kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya UAE, Bahrain na Israel

Sudan pia ni nchi nyingine ya Kiarabu ambayo hivi karibuni imetangaza kuwa imefikia mapatano na utawala wa Kizayuni wa Israel wa kuanzisha uhusiano wa kawaida baina ya pande mbili.

Hatua ya nchi hizo tatu za Kiarabu ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel imekosolewa na kulaaniwa vikali katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Wakati huohuo Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Faisal bin Farhan Al Saud amesisitiza kwa mara nyingine kuhusu msimamo wa nchi yake wa kuunga mkono kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni. Farhan Al Saud alitoa sisitizo hilo jana Jumamosi pembeni ya kikao cha G20 kilichofanyika mjini Riyadh kwa njia ya video.../

 

Tags