Nov 23, 2020 09:40 UTC
  • Saudi Arabia na kikao cha G20

Saudia Arabia hivi karibuni imekuwa mwenyeji wa kikao cha siku mbili cha viongozi wa kundi la G20.

Nchi 19 za Argentina, Australia, Brazil, Canada, China, Ufaransa, Ujerumani, India, Indonesia, Italia, Japan, Mexico, Korea Kusini, Afrika Kusini, Russia, Saudi Arabia, Uturuki, Uingereza na Marekani ndizo zinazounda kundi hilo la G20, ambalo linadhibiti karibu asiliamia 80 ya uchumi wa dunia na kujumuisha thuluthi mbili ya idadi ya watu wote ulimwenguni. Wawakilishi wa Mfuko wa Kimataifa wa Fedha IMF, Benki ya Dunia na Umoja wa Mataifa pia hushiriki katika vikao vya kundi hilo ambavyo hufanyika kila mwaka mara moja.

Kikao cha mwaka huu kimefanyika katika mazingira ambayo vikao vingine vitatu vya awali vilifanyika katika mazingira tatanishi. Kikao cha mwaka 2017 mjini Hamburg Ujerumani na cha 2019 nchini Japan vilifanyika chini ya wingu zito la utata wa siasa za Rais Donald Trump wa Marekani ambaye alizuia mvutano mkubwa na viongozi wa nchi nyingine wanachama wa kundi hilo na hasa Uchina. Kikao cha 2018 pia kilifanyina nchini Argentina huku kukiwa na wingu zito na jeusi la ukatili jinai iliyotekelezwa na Muhammad bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia, dhidi ya mwandishi Jamal Khashoggi akiwa nchini Uturuki.

Kikao cha G20 kilichofanyika Riyadh kwa njia ya video

Saudia Arabia imeandaa kikao cha mwaka huu kwa njia ya video katika mazingira magumu ya kuenea duniani virusi vya corona. Hata kama uandaaji wa kikao hicho ni hatua chanya kwa watawala wa Saudi Arabia lakini ni wazi kuwa kuandaliwa kikao hicho kwa njia ya video kumewanyima fursa na hasa Muhammad Salman, ya kunufaika kisiasa na uwepo wa moja kwa moja wa viongozi wa kundi la G20 nchini kwao. Katika upande wa pili kutohudhuria moja kwa moja viongozi wa kundi hilo kikao hicho huko Riyadh kumeondoa pia fursa ya viongozi wa nchi tofauti kukutana ana kwa ana na kuweza kufanya mazungumzo ya pande mbili au ya pande kadhaa kwa manufaa ya raia wao.

Ajenda kuu ya kikao cha mwaka huu imekuwa ni namna ya kupambana na virusi vya corona na kupunguza athari zake hasi kwa uchumi wa dunia. Ni kutokana na suala hilo ndipo ikasemekana kuwa viongozi wa kundi la G20 katika kikao chao cha karibuni wameamua kutenga dola bilioni 21 kwa ajili ya kukabiliana na corona na dola trilioni 11 kwa lengo la kusaidia na kuunga mkono miradi ya kiuchumi ulimwenguni.

Saudia Arabia ni nchi ya kwanza ya Kiarabu kuandaa kikao cha G0 lakini pamoja na hayo imekabiliwa na ukosolewaji mkubwa. Sehemu ya ukosoaji huo inahusiana na masuala ya miaka mingi iliyopita kuhusu uanachama wa nchi hiyo katika kundi la G20. Wakoasaji wanasema Saudi Arabia kimsingi haina uchumi unaotegemea viwanda bali unategemea pato la mafuta na hivyo haina sifa zinazofaa za kuiwezesha kuwa mwanachama wa kundi hilo la nchi zenye viwanda.

Ukosoaji mwingine unaoelekezwa kwa nchi hiyo ya Kifalme ni kwamba kundi la G20 kimsingi ni kundi la kiuchumi lakini Saudi Arabia inalitumia kundi hilo kwa malengo ya kisiasa na kujaribu kukosha sura yake iliyochafuliwa na jinai, mauaji na ukiukaji wa haki za binadamu. Utawala wa Saudia umekuwa ukikiuka haki za binadamu na kutekeleza jinai za kutisha ndani na nje ya mipaka ya nchi hiyo, hasa katika miaka ya karibuni. Kukamatwa idadi kubwa ya wanaharakati wa masuala ya kisheria na kiraia, wanawafalme wa Saudia, vita vya kichokozi vya karibu miaka 6 dhidi ya Yemen, vita ambavyo vimesabisha maafa makubwa zaidi ya kibinadamu ulimwenguni katika miongo ya karibuni na vilevile kuuliwa kinyama Jamal Khashoggi, mwandishi mashuhuri mkosoaji wa utawala wa Saudia ni baadhi tu ya mifano ya wazi ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na watawala wa Riyadh.

Jamal Khashoggi aliyeuawa kikatili kwa amri ya Muhammad Salman

Kwa msingi huo, kamati ya haki za binadamu ya bunge la Ujerumani imetoa taarifa ikieleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu hali mbaya ya haki za binadamu katika ufalme wa Saudi Arabia na kukosoa vikali vikwazo na kutiwa mbaroni wapinzani wa utawala huo wanaopigania haki za binadamu na kuheshimiwa demokrasia nchini humo. Lujain al-Hadhlul, mwanaharakati wa kike wa Saudia ambaye anahudumia kifungo tokea mwaka 2018 amewataka wanachama wa G20 wawashinikize watawala wa Saudia ili wawachilie huru wafungwa na wanaharakati wanaozuiliwa kinyume cha sheria katika jela za nchi hiyo.

Hali hiyo imezua wasiwasi kwamba badala ya kundi la G20 kushughulikia masua ya uchumi wa dunia, linatumiwa vibaya na baadhi ya nchi zisizohedhimu demokrasia wala haki za binadamu, na hasa Saudi Arabia, kufikia malengo yao ya kisiasa na wakati huohuo kujaribu kusafisha rekodi zao chafu na nyeusi za ukiukaji wa haki za binadamu na jinai.