Nov 23, 2020 12:44 UTC
  • Netanyahu na Pompeo wafanya ziara ya siri kwa wakati mmoja huko Saudia

Duru za Kizayuni zimeripoti kuwa, Waziri Mkuu wa utawala huo Benjamini Netanyahu na baadhi ya maafisa wa Shirika la Ujasusi la Israel (MOSSAD) wamefanya ziara ya siri kwa wakati mmoja na Mike Pompeo Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani nchini Saudi Arabia.

Tovuti ya gazeti la Haaretz la Israel leo Jumatatu imeeleza kuwa, katika safari yake hiyo ya siri nchini Saudi Arabia Benjamin Netanyahu amekutana na kufanya mazungumzo na Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia. Haaretz limeongeza kuwa, Yossi Cohen, mkuu wa shirika la  kijasusi la Israel Mossad ameongozana na Netanyahu katika ziara hiyo ya siri huko Saudia; na alishiriki katika mazungumzo yaliyofanywa na Muhammad bin Salman na Mike Pompeo katika mkoa wa Tabuk nchini humo. 

Muhammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia akutana kwa siri na Pompeo na Netanyahu 

Duru hiyo ya Kizayuni imesisitiza kuwa, katika hali ambayo  safari hiyo ya Waziri Mkuu wa Israel imesajiliwa kwenye tovuti ya kimataifa ya kufuatilia na kusimamia usalama wa ndege (Flight Tracking) lakini ofisi ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni imekataa kutoa maelezo yoyote kuhusu ziara hiyo. Netanyahu amefanya ziara hiyo nchini Saudi Arabia huku Mike Pompeo Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani akiwa katika ziara ya kuzitembelea nchi kadhaa za eneo hili. 

Inaonekana kuwa mazungumzo ya viongozi hao wa Israel, Saudia na Marekani yanajiri katika juhudi za rais wa Marekani, Donalda Trump za kuendeleza mchakato wa kuanzisha uhusiano rasmi kati ya utawala wa Kizayuni na baadhi ya tawala za Kiarabu za eneo hili.