Nov 23, 2020 12:56 UTC
  • WHO yatahadharisha kuhusu kusambaratika mfumo wa afya Ukanda wa Ghaza

Mkuu wa Ofisi ya Shirika la Afya Duniani (WHO) katika Ukanda wa Ghaza ametahadharisha juu ya kusambaratika mfumo wa afya katika eneo la Ghaza.

Abdulnasser Sobh Mkuu wa Ofisi ya WHO huko Ghaza leo ametahadharisha kuwa, kuongezeka kwa kasi idadi ya watu wanaoambukizwa corona katika Ukanda wa Ghaza wiki iliyopita kumezidisha hali ya wasiwasi. Abdulnasser Sobh ameeleza kuwa, kuna uhaba wa suhula za kitiba katika Ukanda wa Ghaza na iwapo hali hiyo itaendelea kushuhudiwa katika eneo hilo mfumo wa afya utashindwa kukidhi mahitaji  kwa zaidi ya wiki mbili na hivyo kusambaratika.  

Ghaza na jitihada za kukabiliana na maambukizi ya corona 

Mkuu wa Ofisi ya Shirika la Afya Duniani katika Ukanda wa Ghaza amesema kuwa shirika hilo limesaidia kuingizwa Ghaza suhula za kitiba zinazohitajika kwa ajili ya kukabiliana na maambukizi ya corona katika eneo hilo; na kwamba hatua kali za udhibiti zinapasa kuchukuliwa ili kukabiliana na corona na kupunguza idadi ya maambukizi miongoni mwa raia wa Palestina wanaoishi  Ghaza. 

Hadi sasa jumla ya watu 14,084 wamepatwa na corona katika Ukanda wa Ghaza huku idadi ya vifo ikiongezeka hadi 92. Israel ililiweka eneo la Ukanda wa Ghaza chini ya mzingiro wa anga, nchi kavu na majini tangu mwaka 2006 na kusababisha masaibu na matatizo chungunzima kwa wakati wa Kipalestina wa eneo hilo.