Nov 25, 2020 02:42 UTC
  • Kuondoka askari wa Marekani nchini Iraq; msimamo wa serikali ya Baghdad na makundi ya mapambano

Katika hali ambayo viongozi wa serikali ya Baghdad wanasema kuwa askari 500 wa Marekani wataanza kutoka katika ardhi ya Iraq miezi miwili ijayo, Sheikh Qais al-Khaz'ali, Katibu Mkuu wa Harakati ya Asaib Ahlul Haq, karibuni hivi alitetea silaha za harakati hiyo ya mapambano ya Kiislamu akisisitiza kuwa muhula wa usitishaji vita na Marekani umekwisha.

Suala la kuondoka askari hao vamizi katika ardhi ya Iraq kwa mara nyingine tena limepamba moto nchini humo katika wiki za hivi karibuni. Mustafa al-Kadhimi, Waziri Mkuu wa Iraq amezungumza kwa njia ya simu na Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani na kuafikiana naye kuhusu suala hilo la kuondoaka askari 500 wa nchi hiyo katika ardhi ya Iraq.

Fuad Hussein, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq amesema kuwa baada ya mazungumzo hayo pande mbili zimekubaliana juu ya kuondoaka askari hao huko Iraq. Christopher Miller, anayesimamia Wizara ya Ulinzi ya Marekani kwa sasa pia alisema Jumanne ya wiki iliyopita kwamba askari wa nchi hiyi walioko Afghanistan na Iraq watapunguzwa ili kufanya idadi ya askari wa Marekani walioko katika kila moja ya nchi hizo kufikia 2500.

Tahsin al-Khafaji, Msemaji wa Kamandi ya Operesheni za Pamoja ya Iraq alisema Jumamosi kwamba askari wa Marekani wanajiandaa kutoka nchini humo na kwamba kwa mujibu wa mapatano yaliyofikiwa kati ya Baghdad na Washington, katika hatua ya kwanza askari 500 wa Marekani wanapasa kuondoka nchini humo.

Pamoja na hayo Sheikh Qais al-Khaz'ali, Katibu Mkuu wa Harakati ya Asaib Ahlul Haq alisema Alkhamisi katika mahojiano na televisheni ya al-Iraqiyya kwamba muhula wa usitishaji vita uliokuwa umewekwa kati ya pande mbili umekwisha kutokana na kutotekelezwa masharti na kwamba sasa makundi ya mapambano ya Iraq yana haki ya kukabiliana kijeshi na askari wa kigeni.

Sheikh Qais al-Khaz'ali

Swali muhimu hapa ni kwamba je, ni masharti gani hayo yaliyokuwepo kati ya makundi hayo na Marekani na ni kwa nini Sheikh Qais al-Khaz'ali anasema hayakutekelezwa? Ameashiria masharti mawili kati ya hayo na kusema uwepo na kuondoka kwa askari wa Marekani nchini Iraq unapasa kufanyika kwa mujibu wa jedwali maalumu linaloainisha wakati maalumu wa kutekelezwa jambo hilo. Anasema sharti la pili ni serikali ya Baghdad kuwa na udhibiti kamili wa anga yake ili isije ikatumika vibaya kwa ajili ya kutekeleza mashambulio mengine yaliyo nje ya sheria.

Hata kama kumetangazwa kuwa askari wa Marekani wataondoka Iraq katika kipindi cha miezi miwili ijayo, lakini ni wazi kuwa suala hilo halijayaridhisha makundi ya mapambo ya nchi hiyo.

Sababu ya kwanza ni kuwa kuondoka adadi hiyo ya askari 500 katika kipindi cha miezi miwili si jambo la kimantiki na kwamba wanaweza kuondoka katika kipindi kifupi sana. Isitoshe kuna uwezekano mkubwa wa askari hao kutoondoka kwa kutilia maanani uwezekano mkubwa wa Donald Trump kutokuwa tena rais wa Marekani mwakani.

Suala la pili ni kuwa hakuna jedwali jingine linaloainisha wakati hasa wa kuondoka askari watakaosalia katika ardhi ya Iraq na tatu ni kwamba kwa mujibu wa kauli ya Fuad Hussein, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq, askari watakaosalia hawatachukuliwa tena kuwa ni askari jeshi wa kupigana bali watakuwa kama raia wa kawaida. Hii ni katika hali ambayo, Mustafa al-Kadhimi aliposafiri Marekani mwezi Agosti uliopita, Trump alimwambia kuwa askari wa nchi hiyo wataondoka Iraq katika kipindi cha miaka mitatu. Kwa maelezo hayo, ni wazi kuwa matamshi ya Fuad Hussein yana maana kwamba kimsingi askari watakaosalia nchini Iraq hawatatakiwa kuondoka karibuni.

Hivyo inaonekana kuwa matamshi ya Sheikh Qais al-Khaz'ali, Katibu Mkuu wa Harakati ya Asaib Ahlul Haq kuhusu kumalizika muhula wa usitishaji vita na Marekani yanailenga moja kwa moja serikali ya Baghdad, ambayo viongozi wake wanatoa matamshi ya kuonyesha kwamba hawana nia yoyote ya kuwaondoa askari wote wa Marekani katika ardhi ya nchi hiyo, bali kwa kutoa idadi ndogo tu wanakusudia kupoteza muda na kupunguza mashinikizo ya makundi ya mapambano ya nchi hiyo na hasa katika wakati huu wa kukaribia kufanyika uchaguzi wa bunge la Iraq ambao umepangwa kufanyika mwezi Juni ujao.

Kituo cha Marekani cha Ain al-Asad nchini Iraq

Katika upande wa pili, kwa kumalizika utawala wa Trump na kuingia madarakani huko White House serikali ya Joe Biden Januari mwakani, kuna uwezekano mkubwa wa kuwekwa tena mezani suala zima la kuondolewa askari wa Marekani walioko Iraq, jambo ambalo halikubaliwi kabisa na makundi hayo ya Kiislamu.

Nukta ya mwisho ni kwamba bunge la Iraq lilipasisha muswada wa kufukuzwa nchini humo askari wa Marekani hapo tare 5 Januari mwaka huu na mamilioni ya raia wa Iraq pia mwishoni mwa mwezi huo huo walifanya maandamano makubwa ya kutaka jambo hilo litekelezwa haraka iwezekanavyo. Kwa msingi huo kufukuzwa nchini humo askari vamizi wa Marekani ni muswada uliopitisha na bunge la taifa na pia ni takwa muhimu la Wairaqi ambalo linapaswa kutekelezwa na kufuatiliwa kwa karibu na serikali ya Baghdad.

Tags