Nov 25, 2020 12:18 UTC
  • Imarati yasitisha kutoa visa kwa raia wa nchi 13 zikiwemo Kenya na Iran

Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) umesitisha kutoa visa ya kuingia nchini humo kwa raia wanaotoka katika nchi 13 ambapo akthari ya mataifa hayo ni ya Kiislamu.

Duru za karibu na utawala wa Umoja wa Falme za Kiarabu zinaeleza kuwa, raia wa nchi ambazo kuanzia sasa hawatapatiwa visa ya kuingia nchini humo ni kutoka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Syria, Somalia, Afghanistan, Libya na Yemen. Nchi nyingine ambazo raia wake hawatapatiwa visa ya kuingia nchini Imarati ni Algeria, Kenya, Iraq, Lebanon, Pakistan, Tunisia na Uturuki.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, marufuku hiyo ya kutotoa visa kwa raia wa mataifa hayo ilianza kutekelezwa tangu juma lililopita. Hata hivyo bado haijafahamika kama marufuku hiyo inajumuisha kila raia wa mataifa hayo anayeingia Imarati au kuna watakaopatiwa visa kutokana na sababu maalumu kama za masomo, tiba au la.

Licha ya kuwa, viongozi wa utawala wa Imarati hawajalizungumzia wazi na hadharani tangazo hili pamoja na sababu za kuchukua hatua hii, lakini chanzo kimoja ambacho hakikutaka kutajwa jina lake kimeeleza kuwa, uamuzi huo umechukuliwa kutokana na sababu za kiusalama.

Makao makuu ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Imarati

 

Duru za ndani zinasema kuwa, uamuzi wa kutowapatia visa ya kuingia Imarati raia wanaotoka katika mataifa hayo ni wa muda.

Pamoja na hayo, uamuzi wa Imarati ambayo hivi karibuni ilitangaza kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel wa kusimamisha utoaji visa kwa mataifa hayo ambayo mengi yao ni ya Kiislamu umezua maswali mengi yasiyo na majibu.