Nov 26, 2020 00:51 UTC
  • Malengo ya habari zenye mgongano kuhusu safari ya Netanyahu Saudi Arabia

Katika muda wa masaa 48 yaliyopita zimetangazwa habari kadhaa zenye kugongana kuhusu safari inayodaiwa kufanywa na waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu nchini Saudi Arabia na kikao cha pande tatu kilichodaiwa kufanywa baina yake na mrithi wa ufalme wa nchi hiyo Mohammad bin Salman pamoja na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo.

Redio ya jeshi la Israel ilikuwa ya mwanzo kutangaza safari ya Netanyahu nchini Saudia na kikao kilichofanyika kati yake na Bin Salman na Pompeo. Kisha likafuatia gazeti la Kizayuni la Jerusalem Post, ambalo lilifichua taarifa nyingine mpya kuhusu safari hiyo ya siri ya waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni nchini Saudi Arabia na likaripoti kwamba, Netanyahu hakumjulisha hata waziri wake wa mambo ya nje Gabi Ashkenazi na waziri wake wa vita Benny Gantz kuhusu safari yake hiyo ya siri. Gazeti hilo liliashiria pia kwamba Yossi Cohen mkuu wa shirika la ujasusi la Israel Mossad aliandamana na Benjamin Netanyahu katika safari hiyo ya Saudia.

Baada ya kutangazwa na vyombo vya Israel, duru za habari za nchi tofauti ziliichangamkia na kuiakisi habari hiyo, lakini maafisa rasmi wa Israel na Saudi Arabia hawakusema chochote kuhusu ukweli wa habari yenyewe. Shirika la habari la Reuters liliripoti kuwa, katika kikao cha ndani ya chama chake cha Likud, Netanyahu alikwepa kutoa maelezo na kujibu masuali kuhusu ukweli wa habari kwamba alikutana na kufanya mazungumzo ndani ya ardhi ya Saudi Arabia na mrithi wa ufalme wa nchi hiyo.

Miongoni mwa vyombo vya habari vilivyoakisi habari ya kikao kinachodaiwa kufanywa kati ya Netanyahu na Bin Salman

Baada ya kubainishwa hisia na maoni tofauti kuhusu habari hiyo, hatimaye waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Faisal bin Farhan Al Saud akaandika ujumbe kwenye mtandao wa Twitter na kukadhibisha taarifa za kufanyika kikao baina ya Netanyahu na mrithi wa ufalme wa nchi hiyo. Kwa hivyo katika hatua ya kwanza, inavyoonekana, kutangazwa habari hiyo ulikuwa mchezo wa vyombo vya habari ulioanzishwa na Wazayuni kwa lengo la kuanzisha vita vya kisaikolojia dhidi ya mhimili wa muqawama na hasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na vilevile kuziaminisiha fikra za waliowengi kwamba serikali ya Trump ingali inaendeleza suala la kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya nchi za Kiarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kuhusiana na nukta hiyo, Nusratullah Tajik, balozi wa zamani wa Iran nchini Jordan anasema: "Kuenezwa habari yenye mgongano kuhusu safari ya Netanyahu nchini Saudi Arabia kumefanywa kwa lengo moja tu la kuichochea Iran, au kwa maneno mengine, kuanzisha vita vya kisaikolojia dhidi yake; na kwa upande mwingine kumetumiwa na Pompeo kwa lengo la kuwachangamsha waitifaki wake wa kikanda."

Nukta nyingine ni ya kujiuliza kwamba, hivi kweli inawezekana kufanywa safari kama hiyo katika wakati huu, ambapo Donald Trump ameshaanza kutekeleza mchakato wa kukabidhi madaraka kwa Joe Biden, yaani katika wakati ambapo muungaji mkono muhimu zaidi wa Bin Salman na Netanyahu anaenguliwa katika uga wa siasa?

Kutoka kushoto: Bin Salman, Trump na Netanyahu

Kuna mitazamo miwili kuhusiana na nukta hii. Mtazamo wa kwanza ni kuwa Mohammad Bin Salman ana uhusiano wa karibu na Trump na Netanyahu; na kimsingi ni kwamba yeye ni mtu mtegemezi na si mwenye kujiamini barabara kwa ajili ya kuchukua maamuzi mazito. Kwa hivyo upo uwezekano kwamba mazungumzo hayo yamefanyika, kwa kuzingatia kuwa yanakidhi maslahi ya wazayuni na kwa kutilia maanani kwamba Bin Salman mwenyewe ana matarajio maalumu kwa uungaji mkono wa lobi ya Kizayuni kwa ajili ya kukalia kiti cha ufalme wa Saudia. Kwa hivyo mchezo wa vyombo vya habari uliochezwa kwa sura ya kuonyesha "utata wa habari" na kutotangazwa msimamo rasmi kuhusu safari hiyo, vimefanywa kwa madhumuni ya kuepusha mashinikizo ya fikra za waliowengi ndani ya Saudia na katika upeo wa kieneo dhidi ya Bin Salman.

Mtazamo mwingine uliopo ni kuwa Benjamin Netanyahu hakufanya safari yoyote huko Saudi Arabia, na kwamba aliyefanya safari kuelekea Riyadh ni afisa wa ngazi ya chini wa utawala wa Kizayuni; na kwa hiyo habari kuhusu safari ya waziri mkuu wa Israel nchini Saudia ni hadithi waliyojitungia Wazayuni kwa utashi wao. Dakta Sayyid Hadi Burhani, mtaalamu wa masuala ya Asia Magharibi anaielezea hivi nukta hiyo: "Wakati Bin Salman na Pompeo walipokutana, Wazayuni walibuni safari hiyo bandia; na kuna uwezekano ilifanyika kweli safari ya ndege iliyotoka ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kwa kisingizio fulani na kuelekea Saudia na hata akawa amepakiwa ndani yake na kupelekwa huko afisa wa ngazi ya chini wa Israel na baadaye akarejeshwa; na Waisraeli wamelitumia suala hilo kufanya mchezo na hadaa ili kwa njia hiyo kuonyesha kwamba, umefanyika mkutano kati ya Netanyahu na Bin Salman. Waisraeli wana rekodi ndefu ya masuala kama haya na wamebobea katika harakati za aina hii." 

Nukta ya kutamatishia uchambuzi huu ni kuwa, bila kujali kama safari ya Netanyahu nchini Saudi Arabia imefanyika au la, makundi ya muqawama hayatiwi hofu wala wasiwasi wowote na jambo hilo, kama ambavyo shambulio la makombora la jeshi na kamati za kujitolea za wananchi wa Yemen dhidi ya kiwanda cha kusafishia mafuta cha Saudia cha Aramco lilifanyika baada ya kupita masaa matano tu ya wakati uliodaiwa kufanyika mazungumzo kati ya Netanyahu na Bin Salman.../