Nov 26, 2020 04:34 UTC
  • Wanawake wa Kipalestina zaidi ya elfu 15 watiwa mbaroni na Israel kuanzia mwaka 1967 hadi sasa

Kituo kimoja cha Utafiti Maalumu wa Masuala ya Mateka wa Kipalestina kimeripoti kuwa, zaidi ya wanawake wa Kipalestina elfu 15 wametiwa mbaroni na utawala wa Kizayuni tangu mwaka 1967 hadi sasa.

Riyadh al Ashqar Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti Maalumu wa Masuala ya Mateka wa Kipalestina jana alieleza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel tangu mwaka 1967 hadi sasa imewatia mbaroni wanawake wa Kipalestina zaidi ya elfu 15 na karibu wanawake wa Kipalestina 2,250 tangu kuanza Intifadha ya al Aqsa mwaka 2000 hadi sasa. Vijana wenye umri mdogo, wagonjwa na wazee ni miongoni mwa wanawake hao wa Kipalestina waliotiwa mbaroni na utawala wa Kizayuni katika kipindi chote hicho tajwa.  

Al Ashqar ameeleza kuwa utawala wa Kizayuni ulishadidisha siasa za kuwatia mbaroni kiholela wanawake wa Kipalestina tangu kuanza vuguvugu la mapambano ya wananchi wa Palestina mwezi Oktoba mwaka 2015 kwa ajili ya kuilinda na kuitetea Quds Tukufu na msikiti wa al Aqsa; na hivi sasa wanawake 39 wa Kipalestina wanaendelea kushikiliwa katika jela za Israel ambapo 14 kati yao ni akinamama wa makumi ya watoto na waliosalia wakiwa ni wanavyuo na wawakilishi wa bunge la Palestina.  

Hujuma za Wazayuni katika msikiti wa al Aqsa  

Ripoti hiyo imeongeza kuwa, utawala wa Kizayuni inatumia visingizio mbalimbali kuwatia mbaroni wanawake wa Kipalestina ikiwa ni pamoja na kuwatuhumu kutuma jumbe katika mitandao ya kijamii dhidi ya Uzayuni, kuwatuhumu kuwa walikuwa na lengo la kutekeleza oparesheni za kimuqawama au kushiriki katika harakati za kuulinda msikiti wa al Aqsa. 

Tags