Nov 27, 2020 06:52 UTC
  • Televisheni nyingine ya Israel nayo yaifanyia istihzai na kejeli Imarati

Kanali moja ya televisheni ya utawala wa Kizayuni imerusha hewani mchezo wa kuigiza wa vichekesho ambao unaukejeli na kuufanyia istihzai Umoja wa Falme za Kiarabu yaani Imarati.

Mtandao wa habari wa al Khalij al Jadid umeweka sehemu moja ya mchezo huo wa kuigiza uliorushwa hewani na kanali ya 11 ya televisheni ya Israel ambapo mmoja wa waigizaji katika mchezo huo amejifanya ni raia wa Imarati.

Katika mchezo huo wa kuigiza, muigizaji wa nafasi ya raia wa Umoja wa Falme za Kiarabu anaonekana kuchanganyikiwa na halafu anauliza, baada ya mimi kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni, nimepata nini? Muigizaji mwingine aliyecheza nafasi ya raia wa utawala wa Kizayuni, anamjibu kwa sauti na lugha ya kejeli na istihzai akimwambia, umesahau kuwa wewe umepewa bure ndege za kivita za F-35, mabomu na vifaru?

Imarati imeamua kutangaza uhusiano na utawala wa Kizayuni bila ya kujali jinai kubwa za utawala huo pandikizi

 

Kabla ya hapo pia, kanali ya 12 ya televisheni ya utawala wa Kizayuni iliwahi kurusha hewani filamu ambayo ndani yake wanaonekana waigizaji wawili, mmoja akijifanya ni waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na mwingine akijifanya ni mrithi wa kiti cha ufalme wa Imarati, Mohammed bin Zayed wakiwa wamekaa kwa sura ya watu waliozama kwenye mapenzi makubwa baina yao huku wakiimba nyimbo ya amani. 

Katikati ya mwezi Septemba mwaka huu, Imarati na Bahrain zilitangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel na kufuatiwa na nchi nyingine ya Kiarabu, Sudan. Hata hivyo hadi leo viongozi wa nchi hizo wameshindwa kusema wamepata nini katika mkabala wa kujidhalilisha kwao huko mbele ya Wazayuni, kiasi kwamba hata televisheni za utawala wa Kizayuni wa Israel sasa zinawafanyia kejeli na istihzai kutokana na kutokuwa na chochote walichopata katika suala hilo.

Tags