Nov 27, 2020 10:17 UTC
  • Kushadidi mizozo na hitilafu katika Baraza la Mawaziri la utawala haramu wa Israel

Hitilafu na mizozo ndani ya Baraza la Mawaziri la utawala haramu wa Israel zingali zinaongezeka na zinaonekana kuchukua mkondo mpya.

Kuanzia Novemba 2018 hadi Machi 30 mwaka huu, walimwengu wameshuhudia mkwamo wa kisiasa huko Israel. Hata kufanyika chaguzi tatu katika kipindi cha mwaka mmoja hakukuweza kupelekea kupatikana mrengo au chama kilichoibuka na ushindi mutlaki ili kiweza kuunda serikali mpya.

Hatimaye baada ya kuibuka virusi vya Corona, Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Israel na ambaye pia ndiye kiongozi wa chama cha Likud akafanikia maafikiano na Benny Gantz kiongozi wa chama cha Blu na Nyeupe ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

Serikali ya sasa ya utawala ghasibu wa Israel ambayo tangu mwanzoni tu mwa kuundwa kwake yaani mwezi Mei mwaka huu, ilikabiliwa na changamoto mbalimbali, lakini changamoto kubwa zaidi ilikuwa ni kugubikwa na anga ya kutoamiana na kutanguliza mbele maslahi ya kimirengo katika utendaji wake. Ukweli wa mambo ni kuwa, tangu katika masiku ya awali tu ya kuundwa serikali hiyo hakukuweko na hali ya kutosha ya kuamianiana baina ya Netanyahu na Benny Gantz na kulikuwa na wasiwasi huu katika kambi ya Gantz kwamba, kutokana na Netanyahu kuwa mwenye uchu wa madaraka, huenda baada ya miezi 18 asikabidhi cheo cha Uwaziri Mkuu kwa Gantz kama ilivyo katika makubaliano yao.

Maandamano dhidi ya Benjamin Netanyahu

 

Hali hii ya kutoaminiana iliongezeka na kushadidi zaidi kufuatia hatua kadhaa zilizochukuliwa na Benjamin Netanyahu ndani ya Baraza la Mawaziri la utawala huo ghasibu. Suala la bajeti ni miongoni mwa mambo makuu yaliyozusha na kushadidisha hitilafu baina ya Netanyahu na mshirika wake katika serikali yaani Benny Gantz.

Hali hii ingali inaendelea kushuhudiwa. Netanyahu hakuwa tayari kushauriana na Benny Gantz hata katika masuala muhimu na nyeti kama makubaliano ya Israel ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na Imarati na Bahrain. Inaelezwa kuwa, Netanyahu hata hakumpa taarifa Benny Gantz kuhusiana na safari yake ya huko Riyadh mji mkuu wa Saudi Arabia.

Hitilafu ya karibuni kabisa kwa mujibu wa mtandao wa Kizayuni wa A24 ni hatua ya Benny Gantz ambaye ni Waziri wa Vita wa Israel ya kupinga ombi la Netanyahu la kujiunga maafisa kadhaa wa kijeshi na safari ya ujumbe wa Israel huko Sudan. Gantz alitangaza kuwa, madhali hakuna hati rasmi ya makubaliano na hali ya kutambuana rasmi pande mbili haipo, kiusalama hana hamu ya kutuma wanajeshi wa Israel huko Sudan. Netanyahu kwa upande wake anataka kulitumia hilo kwa ajili ya kupata kiki ya kisiasa.

Benjamin Netanyahu na Benny Gantz

 

Mizozo na hitilafu ndani ya Baraza la Mawaziri la Israel haikomei tu baina ya Netanyahu na Benny Gantz bali hivi karibuni kuliripotiwa habari ya kuweko mvutano baina ya Netanyahu na mkuu wa majeshi ya utawala huo dhalimu.  Inaelezwa kuwa, Netanyahu hana imani na Aviv Kochavi Mkuu wa Majeshi ya Israel na haipi umuhimu mitazamo ya kamanda huyo wa jeshi katika masuala muhimu ya kiusalama na hakuna ushirikiano wa aina yoyote baina ya pande mbili katika masuala nyeti na muhimu ya kiusalama.

Gazeti la Kizayuni la Haaretz limeandika kuhusiana na sakata hili kwamba, Netanyahu anamuona mkuu wa majeshi Aviv Kochavi kuwa tishio kwa mustakabali wake wa kisiasa na anamtazama kwa jicho la Waziri Mkuu ajaye wa Israel. Ni kwa msingi huo, ndio maana anajitahidi kutosema kitu ambacho Kochavi anaweza kukitumia dhidi yake hapo baadaye katika kinyang’anyiro cha kuwania cheo cha Waziri Mkuu.

Aviv Kochavi, Mkuu wa Jeshi la utawala haramu wa Israel

 

Hali hii ya kutoaminiana imekuwa kubwa kiasi kwamba, licha ya kuenea virusi vya corona, lakini Netanyahu hayuko tayari kulipatia suhula jeshi la utawala huo ghasibu ili likabiliane na virusi hivyo. Katika hali ambayo, Netanyahu hana imani na mkuu wa majeshi Aviv Kochavi na amekuwa akifanya mambo kumdhibiti, Yossi Cohen, Mkuu wa Shirika la Kijasusi la Israel (MOSSAD) yeye anaungwa mkono na Netanyahu na kwa namna fulani Netanyahu anampambanisha Cohen na Kochavi.

Nukta ya mwisho ni kuwa, inaoneakna kwamba, mwisho wa urais wa Donald Trump nchini Marekani na kuja madarakani Joe Biden, kutapelekea kudhoofika nafasi ya Netanyahu katika muundo wa madarakani wa utawala ghasibu wa Israel.

Tags