Nov 27, 2020 12:03 UTC
  • Wabunge Iraq waitaka serikali ijibu mapigo kwa kutowapatia viza raia wa Imarati

Baada serikali ya Imarati kusitisha utoaji viza kwa raia wa Iraq wanaotaka kuingia nchini humo, sambamba na kuwaweka kizuizini katika mazingira ya kutatanisha Wairaqi kadhaa wanaoishi nchini humo, wabunge wa Iraq wameitaka serikali yao isitishe kutoa viza kwa raia wa Imarati pia wanaotaka kuingia nchini humo.

Mukhtar al Musawi, mjumbe wa kamati ya uhusiano wa nje ya bunge la Iraq amesema, kamati hiyo imepokea malalamiko kuhusu raia kadhaa wa nchi hiyo waliokamatwa na kuwekwa kizuizini nchini Imarati na akaongezea kwa kusema, 'tunaitaka wizara ya mambo ya nje ichukue hatua haraka ili kuondolewa utata uliopo kuhusu kadhia hiyo, kufahamika sababu ya watu hao kuwekwa kizuizini na kuratibu mawasiliano na jamaa za watu hao.

Mbunge mwingine wa Iraq Hassan Ali amesema, serikali inapaswa kumwita balozi wa Imarati mjini Baghdad na kumkabidhi taarifa ya malalamiko dhidi ya hatua hiyo iliyochukuliwa na nchi yake.

Amir al Fayez, mbunge wa muungano wa Al Fat-h katika bunge la Iraq amesema, hatua iliyochukua Imarati inaendana na uamuzi iliouchukua hivi karibuni wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel na akabainisha kuwa, uamuzi huo wa Abu Dhabi umehusisha akthari ya nchi zinazopinga kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni na zenye msimamo thabiti kwa suala la Palestina.

Karim al Muhammadawi, ambaye ni mbunge mwingine wa muungano wa Al Fat-h ameikosoa serikali akisema: "kimya cha wizara ya mambo ya nje kwa suala hili kinastaajabisha; na serikali inapaswa ijibu mapigo haraka kwa sababu uamuzi huu wa Imarati hauwezi kutetewa."

Sambamba na hatua ya Imarati ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, siku ya Jumatano, Idara ya Uhamiaji ya nchi hiyo ilitoa waraka maalumu ulioeleza kwamba utoaji viza kwa raia wa nchi 13, akthari yao za Kiislamu ikiwemo Iraq unasitishwa hadi itakapotolewa taarifa nyingine.

Kabla ya taarifa hiyo, afisa mmoja wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iraq alitangaza kuwa wamepokea taarifa zinazooonyesha kuwa maafisa wa Imarati wamewakamata na kuwaweka kizuizini raia kadhaa wa nchi hiyo.../

Tags