Nov 27, 2020 12:31 UTC
  • Maradona akumbukwa kwa kauli yake: Moyoni mwangu mimi ni Mpalestina

Wakati dunia inaomboleza kifo cha nguli wa soka duniani Diego Armando Maradona, watu wengi wanatoa heshima zao kwake na kumuenzi kwa msimamo wake wa wazi wa kuunga mkono mapambano ya ukombozi ya wananchi madhulumu wa Palestina.

Hayati Maradona aliyeaga dunia siku ya Jumatano kwa mshtuko wa moyo wiki mbili baada ya kutoka hospitalini mjini Buenos Aires alikofanyiwa upasuaji wa ubongo, alikuwa akisifika kwa kupinga ubeberu, akiwa ni msoshalisti wa mrengo wa kushoto na muungaji mkono wa harakati za kimaendeleo.

Tangu alipokuwa mwanasoka na hata baada ya kustaafu kabumbu Diego Maradona alikuwa akiunga mkono hadharani na bila kuchelea chochote mapambano ya ukombozi ya wananchi madhulumu wa Palestina.

Mwaka 2012 Maradona alijelezea kama 'shabiki nambari moja wa watu wa Palestina'. "Ninawapa heshima, niko pamoja nao kwa kuwahurumia na ninaiunga mkono Palestina bila kuhofu chochote", alitamka hadharani nyota huyo wa soka wa Argentina aliyeiongoza nchi yake kutwaa kombe la dunia la mwaka 1986.

Maradona akiwa na mashabiki wa Soka wa Palestina

Miaka miwili baadaye, mnamo 2014 wakati utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ulipofanya mashambulio ya kinyama dhidi ya eneo la Ukanda wa Gaza na kuua Wapalestina wasiopungua 3,000 Maradona alionyesha ghadhabu kubwa na kuukosoa vikali utawala huo wa kinyama.

"Inachofanya Israel dhidi ya Wapalestina kinaaibisha", alisema katika taarifa aliyotoa.

Mwaka mmoja baadaye zilienea ripoti kuwa Maradona alikuwa katika mazungumzo na Shirikisho la Soka la Palestina kuangalia uwezekano wa kuinoa timu ya taifa ya soka ya Palestina kwa ajili ya michuano ya kuwania kombe la mataifa ya Asia.

Na mnamo mwezi Julai 2018 alipokutana na Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina mjini Moscow, Russia, hayati Diego Maradona alitangaza tena msimamo wake wa muda mrefu wa kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina aliposema: moyoni mwangu, mimi ni Mpalestina.

Maradona alipokutana na Mahmoud Abbas mjini Moscow

Sami Abu Zuhri, msemaji na kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Muqawama ya Palestina HAMAS ametuma salamu za rambirambi na mkono wa pole kwa familia ya Maradona na mashabiki wake duniani kote.

"Tuna huzuni kubwa kutokana na kifo cha mmoja wa wanasoka wakubwa kabisa, 'Maradona', ambaye anajulikana kwa uungaji mkono wake kwa #Piganio la Palestina, ameeleza Abu Zuhri katika ujumbe alioandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter.../