Nov 28, 2020 08:07 UTC
  • Uturuki yakosoa mpango wa nchi za Kiarabu wa kufungua balozi zao Baitul Muqaddas

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amesema mpango wa nchi za Kiarabu wa kufungua balozi zao katika mji wa Baitul Muqaddas, utadhoofisha uwezekano wa kuundwa nchi ya Palestina.

Cavusoglu ameyasema hayo pembeni ya kikao cha 47 cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC kinachofanyika Niamey, mji mkuu wa Niger.

Amesema, kusitishwa umegaji wa ardhi za Wapalestina kulikofanywa na utawala haramu wa Kizayuni mkabala wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na nchi za Kiarabu ni "hadaa" na akabainisha kuwa, kuundwa nchi huru ya Palestina iliyo kitu kimoja na iliyoungana kijiografia kumekuwa ni jambo lisilowezekana kutokana na sera ya umegaji ardhi inayotekelezwa na Israel.

Hafla ya kusaini mkataba wa kuanzisha uhusiano wa kawaida kati ya Imarati, Bahrain na Israel

Baada ya Imarati na Bahrain kutangaza uamuzi wa kufikia mapatano na utawala wa Kizayuni unaoikalia Baitul Muqaddas kwa mabavu, mnamo tarehe 15 Septemba nchi hizo mbili ndogo za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi zilisaini mikataba ya kuanzisha rasmi uhusiano wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni katika hafla iliyofanyika Ikulu ya White House, mjini Washington na kuhudhuriwa na rais Donald Trump wa Marekani na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain Abdullatif Al Zayani amesema kufunguliwa ubalozi wa nchi hiyo mjini Tel Aviv ndio mpango uliokusudiwa kutekelezwa mnamo siku zijazo na utawala wa Aal Khalifa. 

Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Muhammad Shtayyeh amesema inasikitisha kusikia habari za mazungumzo yanayofanywa na baadhi ya nchi za Kiarabu na utawala wa Kizayuni kwa ajili ya kufunguliwa balozi za nchi hizo katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.../

Tags