Nov 29, 2020 01:30 UTC
  • Malengo ya madai na harakati dhidi ya Iran za pande tatu za Trump, Netanyahu na bin Salman

Baada ya kubainika kushindwa Donald Trump katika uchaguzi wa rais nchini Marekani, kumejiri harakati na kutolewa matamshi mbalimbali; na baadhi ya vyombo vya habari vimetangaza juu ya uwezekano wa Marekani na Israel kuishambulia kijeshi Iran.

Marekani, Israel na Saudi Arabia mara kadhaa zimezungumzia suala la kuishambulia kijeshi Iran katika kipindi cha miaka minne ya kuwepo Donald Trump huko White House. Suala la kutekeleza mashambulizi dhidi ya Iran lilizungumziwa pakubwa baada ya Iran kuitungua ndege ya Marekani isiyo na rubani(droni) katika msimu wa majira ya joto wa mwaka 2019 na pia katika msimu wa baridi kali mwaka huu wa 2020 kufuatia Iran kuilenga kwa makombora kambi ya Marekani ya Ain al Asad huko Iraq; hata hivyo Donald Trump hakuchukua hatua kivitendo na kufanya kosa kama hilo. Hivi sasa kadhia hiyo ya kuishambulia Iran imeibuliwa kwa mara nyingine tena kwa kuzijumuisha pamoja baadhi ya ishara.  

Mark Esper Waziri wa Ulinzi wa Marekani alijiuzulu nafasi hiyo baada ya kutangazwa matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais wa nchi hiyo akifuatiwa na baadhi ya washauri wake ambao  pia wamejiuzulu nyadhifa zao ndani ya Wizara ya Ulinzi. Wakati huo huo hivi karibuni Mike Pompeo Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani amefanya ziara katika eneo la magharibi mwa Asia na kufanya mazungumzo na viongozi wa Imarati, Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni wa Israel.  

Mark Esper, Waziri wa Ulinzi wa Marekani aliyejiuzulu  

Hivi sasa Marekani imetuma ndege 52 za kivita katika eneo hili la magharibi mwa Asia. Inaonekana kuwa, mazungumzo ya pande tatu kati ya Netanyahu, Bin Salman na Pompeo pia yamefanyika katika mji mpya wa Neom huko Saudi Arabia. Kiujumla harakati zote hizo zimepekelea baadhi ya vyombo vya habari kuzitaja kuwa ni ishara kwa ajili ya kutekeleza shambulio dhidi ya Iran kabla ya kumalizika kipindi cha urais wa Donald Trump. 

Hakuna shaka kuwa, Netanyahu na Bin Salman wamekuwa na taathira kubwa kwa nyenendo zisizo za kiakhlaqi na kidiplomasia za Donald Trump katika kipindi cha miaka 4 iliyopita ya uongozi wake. Netanyahu na Bin Salman kwa mara kadhaa walifanya jitihada kumshawishi Trump aishambulie Iran lakini kiu ya Trump ilikuwa ni kupiga picha ya kumbukumbu na viongozi wa Iran katika meza ya mazungumzo kuliko jambo jingine lolote; lengo ambalo ameshindwa kufikia licha hata ya kutumia mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi dhidi ya Iran. 

Hivi sasa si Donald Trump pekee aliyeshindwa uchaguzi huko Marekani bali Benjamin Netanyahu na Bin Salman pia ni washindwa wa uchaguzi huo; pigo ambalo linatishia mustakbali wao katika wigo wa madaraka huko Saudia na Israel. Inaonekana kuwa Bin Salman na Netanyahu wanafanya kila wawezalo ili kujinasua na taathira za matokeo ya uchaguzi wa rais nchini Marekani; na juhudi zao za hivi karibuni kabisa ni kumshawishi Trump aishambulie kijeshi Iran. Tovuti ya habari ya Israel Defence siku ya Alhamisi ilikadhibisha habari ya kuwa tayari jeshi la Israel kwa ajili ya vita na Iran na kuandika: kuenezwa uvumi kama huo katika vyombo vya habari vya Israel kumetokana na hitilafu na vuta nikuvute iliyojitokeza katika uchaguzi wa Marekani hali ambayo muda si mrefu itaikumba Israel pia. 

Muhammad bin Salman na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu  

Pamoja na hayo, hatua zinazochukuliwa na Donald Trump na baadhi ya viongozi wa serikali yake zina lengo la kutilia shaka matokeo hayo ya uchaguzi wa rais wa Marekani zaidi ya kuwa na mwelekeo wa kuishambulia Iran. Katika upande mwingine, hata kama Trump amefanya mabadiliko ndani ya Wizara ya Ulinzi lakini ili kuchukua uamuzi wa kuanzisha vita dhidi ya nchi nyingine inabidi kwanza apate ridhaa na mwafaka wa Baraza la Wawakilishi na Seneti ya Marekani; suala ambalo limeashiriwa pia na tovuti ya habari ya Israel Defence.  

Nukta nyingine muhimu ni kwamba, katika muda wa  chini ya miezi miwili uliosalia hadi kumalizika kipindi cha urais wa Donald Trump serikali na wasomi wa Marekani wanajaribu kudhibiti mienendo na hatua za Trump ili kumuepusha kufanya makosa na kuchukua hatua zisizo za busara. Ni wazi kuwa shambulio lolote dhidi ya Iran litaigharimu pakubwa Marekani. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeidhihirishia serikali ya Marekani uwezo wake wa kiulinzi kwa kuitungua ndege yake isiyo na droni mwezi Juni mwaka jana  na pia shambulio lake  dhidi ya kambi yake ya kijeshi ya Ain al Asad nchini Iraq; shambulio lililotajwa kuwa la kwanza dhidi ya Marekani baada ya Vita vya Pili vya Dunia. 

Mabaki ya Droni ya Marekani iliyotunguliwa na Iran 

 

 

Tags