Dec 01, 2020 10:03 UTC
  • Kupamba moto hitilafu za kiintelijensia baina ya Saudia na Imarati katika vita vya Yemen

Baada ya kuibuka hitilafu za kisiasa na kijeshi baina ya Saudi Arabia na Imarati katika vita huko nchini Yemen, sasa kumezuka mzozo baina ya vituo vya kiintelijensia vya pande mbili hizo.

Vita dhidi ya Yemen vilianza Machi 26, 2015. Wahusika wakuu katika vita hivyo ambavyo vimeingia katika mwezi wa 69 ni Saudi Arabia na Imarati. Baada ya kupita mwaka mmoja tangu kuanza vita hivyo, hitilafu na mivutano baina ya Abu Dhabi na Riyadh zilidhihirika wazi. Chimbuko halisi la hitilafu hizo lilihusiana na ‘uga wa ushawishi’ ndani ya Yemen.

Imarati iligeuka haraka mno na kuwa hasimu na mshindani wa Saudi Arabia nchini Yemen kwani Abu Dhabi ilielekeza zaidi nguvu zake katika kisiwa cha kistratejia cha Socotra na kufanya juhudi za kukidhibiti kisiwa hicho. Licha ya kuwa awali Saudia ilipinga harakati hizo za Imarati, lakini ili iweze kuiridhisha iwe pamoja nayo katika vita hivyo, haikuwa na budi isipokuwa kuridhia ushawishi huo wa Imarati.

 

Mbali na ushawishi wa kijiografia, pande mbili hizo ziliingia katika mzozo mkubwa wa ushawishi wa kisiasa. Imarati ilikuwa ikitaka kuwepo wa watu wake wa karibu ndani ya baraza la mawaziri la Abdurabbuh Mansur Hadi. Hata hivyo suala hilo lilipingwa na Mansur Hadi mwenyewe rais aliyejiuzulu wa Yemen pamoja na Saudi Arabia. Kwa muktadha huo, Imarati ikaasisi Baraza la Mpito la Kusini nchini Yemen na likamfanya Aidarous al-Zoubaidi, gavana aliyeuzuliwa wa Aden kuwa kiongozi wa baraza hilo.

Filihali, baraza hili sio tu kwamba, ni mshindani muhimu wa serikali iliyojiuzulu ya Abdurabbuh Mansur Hadi bali limeunda serikali katika eneo hilo ambayo inaonekana kuwa na nafasi bora zaidi kisiasa na kijeshi kulinganisha na serikali ya Mansur Hadi. Hali hii imepelekea kuibuka mapigano makubwa baina ya mamluki wa utawala wa Saudia na Imarati kusini mwa Yemen. Mkoa wa Abyan ulioko kusini mwa Yemen kwa sasa ndio kitovu cha mapigano ambapo kwa akali makumi ya wapiganaji wa pande mbili wameuawa na kujeruhiwa katika mapigano hayo.

Majeshi ya Imarati nchini Yemen

 

Mzozo baina ya Imarati na Saudia hivi sasa umechukua mkondo mpana zaidi na kuingia katika uga wa masuala ya kiusalama na kiintelijensia.  Mtandao wa Khalij Online hivi karibuni uliripoti habari ya kuweko hitilafu za siri baina ya vituo vya kiintelijensia vya Saudia na Imarati na kuandika kuwa, kamandi ya kikosi cha Saudia katika muungano vamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen inataka kupangwa na kuratibiwa upya mamlaka ya vituo vya kiusalama vya nchi shiriki katika muungano huo hususan Imarati.

Majimui ya hitilafu hizi hususan katika uga wa masuala ya kiusalama yamepelekea kuongezeka hali ya kutoaminiana baina ya Abu Dhabi na Riyadh katika vita vyao nchini Yemen. Hali hii ya kutoamiana imekuwa kubwa kiasi kwamba, shirika la  kijasusi la Saudia nchini Yemen limemjuza Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia kwamba, shirika la kijasusi la Imarati likiwa na lengo la kuyakwamisha makundi yenye mfungamno na jeshi la serikali iliyojiuzulu ya Yemen, kwa makusudi kabisa limekuwa likitoa taarifa za upotoshaji kwa vikosi vya kijeshi hususan vikosi vya anga.

Baraza la Mpito la Kusini mwa Yemen

 

Katika upande mwingine sambamba na kuongezeka hitilafu za kiintelijensia, kupata pigo kirahisi muungano vamizi wa Saudi Arabia katika vita nako kumeongezeka mno. Licha ya kuwa uwezo wa makombora wa jeshi na kamati za kujitolea za wananchi wa Yemen baada ya kupita muda umeongezeka na hata kuweza kuvurumisha makombora na kutuma ndege zisizo na rubani ndani ya ardhi ya Saudia, lakini shirika la kijasusi la Saudia linaamini kuwa, kuongezeka hitilafu baina yake na Imarati kumekuwa na taathira hasi katika kushadidisha kupata pigo muungano huo kutoka kwa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa.

Inaonekna kuwa, Imarati inafanya hima ya kujitenga na masuala ya kijeshi vitani na hivyo kuongeza ushawishi wake wa kisiasa na kijiografia nchini Yemen, ili kwa njia hiyo iwepo nchini Yemen kama mshindani na hasimu wa utawala wa Riyadh.

Tags