Dec 02, 2020 11:08 UTC
  • Wasudani kumshtaki Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Abu Dhabi katika mahakama ya ICC

Mshauri wa masula ya kisheria wa faili la kesi ya vijana 80 wa Kisudani ambao walitumiwa vibaya na kampuni ya Black Shield Security Services ya Imarati na kutumwa katika vita nchini Libya bila ridhaa yao amesema kuwa, wanapanga kuwashtaki maafisa kumi wa Imarati akiwemo Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Abu Dhabi katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai.

Omar al-Abid, mshauri wa kisheria wa vijana wa Kisudani ambao walihadaiwa na kampuni ya  Black Shield Security Services  ya Imarati  amesema kuwa, tayari wameanzisha mchakato wa kuwasilisha kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC dhidi ya viongozi na maafisa 10 wa Imarati akiwemo Muhammad bin Zayed al-Nahyan ambaye ni Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Abu Dhabi.

Aidha amesema kuwa, tayari wamelijulisha Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch kuhusiana na hadaa iliyofanywa na kampuni ya Black Shield Security Services  ya Imarati  dhidi ya vijana hao wa Kisudani.

Wasudan wakiandamana kudai haki zao baada ya kuhadaiwa na kampuni ya Black Shield Security Services  ya Imarati 

 

Vijana wa Kisudan waliorejea makwao mwanzoni mwa mwaka huu walisimulia jinsi walivyohadaiwa na kampuni ya Black Shield Security Services iliyowaahaidi kuwapa kazi za ulinzi na badala yake walijikuta wakipewa mafunzo ya kijeshi yasiyooana na kazi zao na kupelekwa bila ya kujua huko Libya na Yemen kupigana vita.

Mwishino mwa mwezi Disemba mwaka jana taasisi moja ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu ililaani vikali hatua ya Umoja wa Falme wa Kiarabu (Imarati) ya kuwaajiri mamluki wa Kisudani wanaotumiwa kupigana bega kwa beba na mbabe wa kivita wa Libya, Jenerali Khalifa Haftar dhidi ya serikali iliyotambuliwa rasmi na jamii ya kimataifa yenye makao yake mjini Tripoli.