Dec 02, 2020 11:09 UTC
  • Ayatullah Issa Qassim: Matokeo ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel ni hatari na ni majanga

Kiongozi wa juu wa kidini wa Waislamu wa Kishia nchini Bahrain amesema kuwa, matokeo ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel yatakuwa hatari na yatasababisha majanga.

Ayatullah Issa Qassim ambaye pia ni Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Bahrain ameeleza kwamba, baadhi ya tawala za Kiarabu zilizoanzisha uhusiano wa kawaida na adui Mzayuni zimejitenga na wananchi wao na kukimbilia kwa Marekani na Israel na kukabidhi hatima ya mataifa yao mikononi mwa tawala hizo kandamizi.

Sheikh Issa Qassim ameongeza kusema kuwa, kudhalilika mataifa yaliyoanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel kumedhihirika haraka mno ikiwa ni muda mfupi tu baada ya viongozi wa mataifa hayo kutia saini makubaliano ya usaliti.

Baada ya Imarati na Bahrain kutangaza kuwa zimeafiki kuutambua rasmi utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, mnamo tarehe 15 Septemba, nchi hizo mbili za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi zilisaini rasmi mkataba wa kuanzisha uhusiano wa kawaida wa kidiplomasia na utawala huo unaoikalia Quds tukufu kwa mabavu, katika hafla iliyofanyika Ikulu ya White House, mjini Washington na kuhudhuriwa na rais Donald Trump wa Marekani na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Ayatullah Issa Qassim, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Bahrain

 

Sudan pia ni nchi nyingine ya Kiarabu ambayo hivi karibuni ilitangaza kuwa imefikia mapatano na utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuanzisha uhusiano wa kawaida baina ya pande mbili.

Hatua ya nchi hizo tatu za Kiarabu ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel imeendelea kukosolewa na kulaaniwa vikali katika Ulimwengu wa Kiislamu.