Dec 03, 2020 07:33 UTC
  • Baraza Kuu la UN lapitisha maazimio matano kuunga mkono Palestina na miinuko ya Golan ya Syria

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha maazimio matano ya kuunga mkono Palestina na miinuko ya Golan ya Syria.

Katika kikao kilichofanywa jana usiku kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Watu wa Palestina, ambayo iliadhimishwa Novemba 29, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha maazimio matano yaliyopendekezwa kwa ajili ya kuiunga mkono Palestina na miinuko ya Golan ya Syria.

Kwa kupitisha maazimio hayo matano, Baraza Kuu la UN lilitangaza upinzani wake kwa hatua za ukaliaji ardhi kwa mabavu zinazochukuliwa na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Katika azmio la kwanza kuhusu miinuko ya Golan ya Syria, azimio hilo limesisitiza tena kuwa Golan ilivamiwa na kuanza kukaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni tangu mwaka 1967.

Azimio jengine la kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitishwa na kamati ya utekelezaji wa haki zisizokanushika za watu wa Palestina ambalo limesisitiza kuhusu jukumu na wajibu wa kudumu wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na kadhia ya Palestina hadi itakapopatiwa ufumbuzi. Azimio hilo limeitaka kamati hiyo kufanya kila iwezalo kuhakikisha haki za Wapalestina zinapatikana.

Image Caption

Azimio la tatu la Baraza Kuu la UN lilihusu kuwepo kwa kitengo maalumu kuhusu haki za Wapalestina katika Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa.

Azimio jengine lililopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilihusu kutatuliwa kwa amani suala la Palestina. Katika azimio hilo, Baraza Kuu la UN limesisitiza kuwa ujenzi wa vitongoji na hatua zote za upande mmoja zinazochukuliwa na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa shabaha ya kubadilisha demografia na muundo wa idadi ya watu katika mji wa Baitul Muqaddas unaokaliwa kwa mabavu na Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan ni kinyume cha sheria.

Kikao hicho cha Baraza Kuu la UN kilipitisha pia azimio la kuanzishwa kitengo maalumu cha habari kuhusu kadhia ya Palestina chini ya kitengo kikuu cha habari kilichoko katika Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa.../